Waziri Mkuu wa Palestina: Wapalestina wanataka uhuru na si sadaka
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54363-waziri_mkuu_wa_palestina_wapalestina_wanataka_uhuru_na_si_sadaka
Waziri Mkuu wa Palestina amesema kuwa mhandisi na mtayarishaji wa mpango wa Kimarekani wa eti amani ya Mashariki ya Kati wa Muamala wa Karne unaosimamiwa na mkwe wa Rais Donald Trump, Jared Kushner na wenzake hawaelewi kuwa Wapalestina hawataki sadaka bali wanadai haki zao za kuwa huru na kukomeshwa uvamizi wa Israel na udhibiti wa dola hilo haramu wa maisha na uchumi wao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 25, 2019 22:27 UTC
  • Waziri Mkuu wa Palestina: Wapalestina wanataka uhuru na si sadaka

Waziri Mkuu wa Palestina amesema kuwa mhandisi na mtayarishaji wa mpango wa Kimarekani wa eti amani ya Mashariki ya Kati wa Muamala wa Karne unaosimamiwa na mkwe wa Rais Donald Trump, Jared Kushner na wenzake hawaelewi kuwa Wapalestina hawataki sadaka bali wanadai haki zao za kuwa huru na kukomeshwa uvamizi wa Israel na udhibiti wa dola hilo haramu wa maisha na uchumi wao.

Mohammad Shtayyeh ambaye alikuwa akizungumzia mkutano wa kuzindua mpango huo wa Kimarekani ulioanza jana nchini Bahrain amesema katika Makala yake iliyochapishwa na gazeti la Washington Post kwamba, wanasiasa na wawekezaji wa Kipalestina wameamua kususia mkutano huo kwa sababu Rais wa Marekani, Donald Trump aliamua kuipendelea Israel tangu aliposhika madaraka na suala hili linaonesha kuwa, serikali yake haiwezi kuwa mpatanishi katika mazungumzo ya amani.

Waziri Mkuu wa Palestina ameeleza hatua kadhaa zilizochukuliia na serikali ya Donald Trump katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ambazo amesema ni vita dhidi ya Wapalestina ikiwa ni pamoja na kuitambua Quds kuwa ni mji mkuu wa Israel, kuhamishia ubalozi wa Marekani katika mji huo unaokaliwa kwa mabavu, kufunga ofisi ya mwakilishi wa Palestina mjini Washington na kusimamisha misaada ya Marekani kwa raia wa Palestina ikiwa ni pamoja na misaada iliyokuwa ikitolewa na nchi hiyo kwa wakala wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wapalestina, UNRWA.

Trump, Netanyahu na Jared Kushner

Mohammad Shtayyeh amesisitiza kuwa Jared Kushner na walioshirikiana naye kubuni mpango eti wa amani baina ya Israel na Wapalestina hawaelewi kuwa haiwezekani kuwanunua au kuwahonga Wapalestina ili wakubali kitu chochote kile kisichokuwa uhuru kamili na haki zao. Ameongeza kuwa, kizimba cha dhahabu kilichoko kwenye akili ya Koshner na Waziri Mkuu wa Israel kinabakia kuwa kizimba kwa Wapalestina.

Waziri Mkuu wa Palestina amesema kuwa, mpango wa amani uliobuniwa na Marekani hauna kipengee chochote kinachotaka kuundwa dola huru la Palestina, hauitaki Israel kuwapa Wapalestina haki zao na zaidi ni kwamba, ni mpango wa ubaguzi wa kizazi wa Trump na Netanyahu na si mpango wa amani.