Mlinzi binafsi wa Mfalme wa Saudia apigwa risasi na kuuawa
Mlinzi binafsi wa mfalme wa Saudi Arabia, Meja Jenerali Abdulaziz al Faghem ameuawa katika kile kilichotajwa kuwa 'hitilafu za kibinafsi'.
Vyombo vya habari vya Saudia vimetangaza leo Jumapili kuwa, al Faghem alipigwa risasi na kuuawa katika tukio ambalo limejiri mjini Jeddah.
Vyombo vya habari vya Saudia vimetangaza kuwa al Faghem ameuawa na rafiki yake kutokana na hitilafu za kibinafsi.
Al Faghem alikuwa mlinzi binafsi wa Mfalme Abdullah wa Saudia na alipofariki aliteuliwa tena kuwa mlinzi wa Mfalme Salman ambaye alimpa cheo cha Meja Jenerali mwaka 2017.
Mwandishi habari wa Saudia Ali Al Ahmad ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa al Faghem alifutwa kazi siku chache zilizopita na hivyo jambo hilo limetilia shaka sababu za kifeo chake.
Amesema siku chache zilizopita al Faghem alionekana akitembea peke yake katika mitaa ya Jeddah jambo ambalo si la kawaida kwa mtu wa cheo chake.
Katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la mauaji ya wapinzani nchini Saudi Arabia hasa baada Mohammad bin Salman kuteuliwa kuwa mrithi wa kiti cha ufalme, hatua ambayo imepingwa na wengi katika nchi hiyo. Bin Salman ambaye anapata uungaji mkono wa Marekani na Israel ameamuru kukamatwa au kuuawa idadi kubwa ya wapinzani wake wakiwemo wafanyabiashara, wanazuoni wa kidini, wanawafalme na wanaharakati wa haki za kiraia.