Makumi ya mateka wa Kipalestina wameuawa kwa mateso Israel
Kundi la kutetea haki za binadamu la Palestina limeripoti kuwa, makumi ya mateka na wafungwa wa Kipalestina wameuawa kwa mateso na ukatili wa aina mbalimbali wakihojiwa na kusailiwa na maafisa wa magereza na jela za utawala haramu wa Israel.
Klabu ya Wafungwa wa Kipalestina (PPC) imeripoti kuwa, mamlaka za Israel zinatumia mbinu mbalimbali za mateso ikiwa ni pamoja na mateso ya kimwili na kinafsi dhidi ya wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za utawala huo na kuwadhalilisha wakati wa kuwahoji kwa ajili ya kuwalazimisha kukiri makosa ambayo hawakufanya. PPC imeashiria mauaji ya Arafat Jaradat aliyeaga dunia katika jela ya Megiddo siku tano tu baada ya kukamatwa na sakari wa Israel kutokana na mateso makali.
Ripoti hiyo pia imesema askari wa Israel waliopewa mafunzo ya vita vya mjini maarufu kwa jina la Nahshon, mwaka 2014 walimuua mfungwa Ra'ed al-Ja'bari baada ya kumnyanyasa kimwili.
Wakati mwingine mateka na wafunwga hao wa Kipalestina hunyimwa usingizi kwa masaa 20, kuwatesa kwa kuwaweka maneo yenye joto na baridi kali sana au kuwekwa kwenye maeneo yenye sauti kubwa kupindukia.
Zaidi ya Wapalestina elfu saba wanashikiliwa katika magereza na jela za Israel na baadhi yao wanashikiliwa kwa zaidi ya miaka 11 bila ya kufikishwa mahakamani.
Ripoti zinasema kuwa, wabunge 13 ni miongoni mwa maelfu ya Wapalestina wanaoshikiliwa katika korokoro za utawala wa Kizayuni wa Israel.