Utabiri wa Sayyid Nasrullah watimia, Marekani yawasaliti Wakurdi wa Syria + Video
Wanamgambo wa Kikurdi wa kaskazini mwa Syria wameilalamikia vikali Marekani kwa kuwasaliti na kuwatelekeza katika mashambulizi ya jeshi la Uturuki dhidi yao, suala ambalo limethibitisha ukweli wa utabiri wa Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah alioutoa takriban miaka miwili iliyopita.
Jana usiku jeshi la Uturuki lilianzisha mashambulizi dhidi ya maeneo ya Wakurdi kaskazini mwa Syria baada ya Marekani kutangaza hiyo jana kwamba, haina nia ya kukabiliana kijeshi na Uturuki iwapo itashambulia maeneo ya wanamgambo hao wa Kikurdi.
Baada ya kutangazwa msimamo huo wa Marekani, wanamgambo wa Kikurdi wanaojiita Syrian Democratic Forces (SDF) wamesema kuwa, Marekani imewasaliti na imewatelekeza mbele ya mashambulizi ya Uturuki.
Karibu miaka miwili iliyopita, yaani tarehe 16 Februari 2018, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon aliwatahadharisha Wakurdi wa Syria akiwaambia kwamba wasiiamini Marekani kwani haina mwamama hata kidogo, bali wanachopaswa kufanya ni kutatua masuala yao na serikali ya Syria kabla ya Marekani haijawasaliti na kuwatelekeza.
Aidha aliwatahadharisha Wakurdi hao kwa kuwaambia kwamba Marekani inawatumia tu katika siasa zake za kukabiliana na Russia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwamba siku itakapoona haifaidiki nao tena itawapiga teke na kuwaacha peke yao.
Baada ya hotuba hiyo, baadhi ya vyombo vya habari vya wapinzani wa Syria vilimfanyia istihzai Sayyid Hassan Nasrullah na walitengeneza Hashtag ndani ya mitandao ya kijamii wakiandika: #Marekani yawasaliti waitifaki wake. Hivi sasa lakini utabiri huo wa Sayyid Hassan Nasrullah umetimia, hasa baada ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon kusema kuwa imeamrishwa iondoke Syria. Kabla ya hapo rais wa Marekani, Donald Trump alikuwa amesema, wakati umefika wa kumalizwa vita vya Syria ambavyo ni vya kikabila na haviihusu ndewe wala sikio Marekani.