Mkataba wa kiusalama wa kieneo; hitajio la Ukanda wa Asia Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56636-mkataba_wa_kiusalama_wa_kieneo_hitajio_la_ukanda_wa_asia_magharibi
Kuendelea kushuhudiwa vita na ukosefu wa amani na usalama katika eneo la Asia Magharibi, kumepelekea kuongezeka mapendekezo ya kuweko mkataba wa kiusalama wa kieneo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2019 06:09 UTC
  • Mkataba wa kiusalama wa kieneo; hitajio la Ukanda wa Asia Magharibi

Kuendelea kushuhudiwa vita na ukosefu wa amani na usalama katika eneo la Asia Magharibi, kumepelekea kuongezeka mapendekezo ya kuweko mkataba wa kiusalama wa kieneo.

Katika miongo ya hivi karibuni eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) limeshuhudia vita, machafuko na hali ya mchafukoge kuliko wakati mwingine wowote ule. Hali hii ina sababu mbalimbali ambazo baadhi yake ni za ndani na nyingine ni za nje ya eneo hili. Kwa upande wa sababu za ndani, ni kuwa kiasili eneo la Asia Magharibi ni la migogoro na mizozo.

Profesa Barry Buzan, mwananadharia wa masuala ya mahusiano ya kimataifa anasema kuwa, utumiaji mabavu upo katika dhati na asili ya eneo la Asia Magharibi. Muundo wa baadhi ya nchi uliofanywa na ukoloni wa Wamagharibi katika karne ya 20, uwepo wa utajiri wa nishati katika eneo hili na kadhalika kuasisiwa utawala bandia wa Israel katika eneo hili ni miongoni mwa sababu za ndani za kuweko vitendo vya utumiaji mabavu na vita katika eneo la Asia Magharibi.

Kwa upande wa sababu za nje, sababun kuu yenye taathira katika kuibuka na kuenea vita na machafuko katika Asia Magharibi ni uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya eneo hili na kufungamana usalama wa baadhi ya watawala na himaya ya madola hayo.

Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu

Licha ya kuwa, vurugu na machafuko katika eneo la Asia Magharibi vimechukua mkondo wa kuongezeka na kushadidi na kutokea maafa ya kibinadamu kama yale yanayoshuhudiwa nchini Yemen, lakini si tu kwamba, hakujaanzishwa mkataba wowote wa kiusalama baina ya nchi za eneo hili, bali kimsingi kukinzana na kugongana maslahi ya madola ya eneo inatajwa kuwa sababu kuu na muhimu ya kuibuka na kusambaa mizozo na vitendo vya utumiaji mabavu katika eneo hili.

Kwa kuzingatia hali hii, tangu awali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitoa pendekezo la kuanzishwa mkataba wa kiusalama wa kieneo. Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ametoa pendekezo la kuweko mkataba wa kutoshambuliana wala kuingilia masuala ya ndani ya upande mwingine. 

Muhammad bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar akihutubia Jumamosi iliyopita katika mkutano wa 'Siasa za Kimataifa' uliofanyika nchini Morocco alizungumzia ombi la Amir wa nchi hiyo Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani  na kuundwa na kutiwa saini mkataba wa kiusalama wa kieneo kwa minajili ya usalama wa eneo la Asia Magharibi na kutiwa saini hati ya makubaliano ya usalama wa kieneo kwa mujibu wa misingi ya usalama na kiakili na kupatikana usalama kwa shabaha ya kuleta amani na ustawi.

Muhammad bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Qatar

Kabla ya hapo pia, Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani akihutubia katika mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alikkuwa amezungumzia suala la mkataba wa kiusalama wa eneo. Aidha Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasilisha mpango mpya wa amani katika eneo la Ghuba ya Uajemi ambao unajulikana kama 'Ubunifu wa Amani wa Hormuz' kwa kifupi HOPE katika hotuba yake kwenye mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mjini New York.

Hapana shaka kuwa, kutiwa saini mkataba wa kutoshambuliana au mkataba wa usalama wa kieneo kunaweza kuwa sababu ya kupatikana hali ya kuaminiana katika eneo hususan baina ya madola makubwa ya eneo. Hali ya kuaminiana ni kitu kilichotoweka kabisa baina ya nchi za Asia Magharibi hususan baina ya madola makubwa ya eneo hili.

Rais Hassan Rouhani akihutubia  mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Ukweli wa mambo ni kuwa, kuongezeka hali ya kuaminiana katika mahusiano ya nchi maana yake ni kuongeza usalama na kupungua mizozo, mivutano na vitendo vya utumiaji mabavu katika eneo na wakati huo huo, hilo litapelekea kupungua utegemezi na usalama wa kuyategemea madola ya kigeni.

Kimsingi ni kuwa, usalama wa kutegemea madola yaliyoko nje ya eneo hili ni moja ya matatizo yanayolikabili eneo la Asia Magharibi kwa sasa na ambalo lina mfungamano na maslahi ya madola makubwa. Jambo hili si tu kwamba, halijaliletea usalama eneo la Asia Magharibi bali limekuwa kikwazo na kizingiti kwa nchi za eneo hili katika njia ya kuwa na mitazamo inayozingatia maslahi  na manufaa yao ya pamoja.