Maandamano ya kupinga serikali yaendelea nchini Lebanon
Maandamano ya kupinga serikali ya wananchi wa Lebanon yameendelea leo kwa waandamanaji kukusanyika karibu na ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge la nchi hiyo katika mji mkuu Beirut.
Waandamanaji wanaolalamikia hali ya uchumi na maisha, ambao waliingia mabarabarani kuanzia jioni ya jana, leo walikusanyika karibu na ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Saad Hariri wakitoa nara na kaulimbiu za kupinga serikali.
Idadi kadhaa ya waandamanaji walikusanyika pia mbele ya "Baitul-Wasat", makazi ya Waziri Mkuu huyo wa Lebanon.
Mashule na mabenki yote leo yalifungwa nchini humo.
Miji mbali mbali ya Lebanon na hasa mji mkuu Beirut tangu jana jioni imekuwa ikishuhduia maandamano ya kupinga serikali ya wananchi wanaolalamikia utendaji dhaifu wa serikali ya Saad Hariri kuhusiana na hali ya maisha na uchumi pamoja na kodi mpya zilizotangazwa na serikali hiyo.
Wiki mbili zilizopita pia Beirut na miji mingine kadhaa ya Lebanon ilikuwa uwanja wa maandamano ya kupinga serikali.
Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Ndani Riya al-Hassan amesema, vikosi vya usalama vimeagizwa kutokabiliana na waandamanaji. Aidha ametoa mwito kwa vyama na mirengo yote serikalini kuungana na kuwa kitu kimoja katika kuunga mkono hatua za kujikusuru kiuchumi zinazochukuliwa na serikali hiyo.../