Matukio yanayojiri Iraq; harakati inayofuata njia tata zaidi na muelekeo usiotabirika
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i56831-matukio_yanayojiri_iraq_harakati_inayofuata_njia_tata_zaidi_na_muelekeo_usiotabirika
Matukio yanayojiri nchini Iraq yanaelekea kwenye njia tata zaidi na muelekeo usiotabirika, kufuatia safari ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani nchini humo na msimamo wa wapinzani wa serikali wa kufanya maandamano Ijumaa ya leo ya tarehe 25 Oktoba.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 25, 2019 02:32 UTC
  • Matukio yanayojiri Iraq; harakati inayofuata njia tata zaidi na muelekeo usiotabirika

Matukio yanayojiri nchini Iraq yanaelekea kwenye njia tata zaidi na muelekeo usiotabirika, kufuatia safari ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani nchini humo na msimamo wa wapinzani wa serikali wa kufanya maandamano Ijumaa ya leo ya tarehe 25 Oktoba.

Tukiyaangalia matukio yanayotokea hivi sasa huko Iraq tutabaini kuwa, hali ya mambo katika nchi hiyo ya Kiarabu na Kiislamu si shwari, bali ni tete na ya hamkani. 

Kuna nukta tano za kutafakari kuhusiana na yale yanayoendelea kujiri nchini Iraq; ya kwanza ikiwa ni ripoti iliyotolewa na kamati iliyochunguza machafuko yaliyotokea hivi karibuni nchini humo.

Maandamano ya kualamikia serikali yaliyofanyika karibuni nchini Iraq

Ripoti ya kamati hiyo imeeleza kwamba, katika maandamano ya kulalamikia serikali, raia 107 waliuawa na wengine 3,458 walijeruhiwa, ilhali hakukuwa na amri yoyote rasmi iliyokuwa imetolewa na viongozi wa ngazi za juu ya kuwafyatulia risasi waandamanaji. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maafa yaliyotokea ya roho za watu yalisababishwa na utumiaji nguvu kupindukia, silaha moto na usimamizi mbovu wa baadhi ya maafisa waliokuweko katika medani za maandamano hayo.

Mbali na ripoti hiyo kukiri kwamba kuna uzembe uliofanywa na baadhi ya vyombo vya usalama, imebainisha pia kuwa, vikosi vya baadhi ya vyombo vya dola viliwafyatulia risasi baadhi ya watu waliohusika na uvunjaji sheria; na kwamba maafisa waliovichochea vikosi vya usalama kutumia mabavu dhidi ya waandamanaji wamefikishwa mbele ya vyombo vya sheria, na tayari makamanda 10 wa ngazi za juu wa operesheni za usalama na wa intelijensia wameshauzuliwa.

Nukta ya pili inahusu msimamo uliotangazwa na muungano wa Nasr, unaoongozwa na Haidar al Abadi, waziri mkuu wa serikali iliyopita ya Iraq kwa ripoti hiyo ya kamati ya uchunguzi.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Iraq, Haidar al Abadi

Baada ya kutolewa matokeo ya uchunguzi huo, muungano wa Nasr umeikosoa ripoti hiyo ukidai kwamba haitoshi. Inavyoonekana, badala ya kuonyesha uungaji mkono kwa waandamanaji, msimamo huo umelenga zaidi kulipiza visasi vya kisiasa na kuikomoa serikali ya Waziri Mkuu Adil Abdul-Mahdi sambamba na kuuchochea na kuukoleza moto wa maandamano ya upinzani dhidi ya serikali. 

Msimamo huo umeonyeshwa, ilhali maandamano ya kupinga serikali au ya kulalamikia hali ya kiuchumi na kijamii yalifanyika pia kwa muda wa miaka mitatu mtawalia wakati wa serikali ya Haidar al Abadi, lakini hayakusaidia kupunguza matatizo ya wananchi wa Iraq.

Nukta ya tatu ya kuitafakari ni unga'ng'anizi wa kamati ya kuratibu maandamano ya kupinga serikali, ya kuitisha maandamano hayo leo Ijumaa. Wakati huohuo Muqtada Sadr, kiongozi wa harakati ya Sadr, naye pia amewataka wafuasi wake washiriki kwenye maandamano hayo ya leo.

Kiongozi wa harakati ya Sadr, Muqtada Sadr

Wito huo wa Muqtada Sadr umekabiliwa na ukosoaji wa kamati ya kuratibu maandamano, ambayo imesisitiza kuwa, mrengo wa Sadr ni sehemu ya serikali iliyoko madarakani, hivyo hauna haja ya kuingia barabarani kuandamana, kwa sababu, kwa kutumia mamlaka ya kisheria uliyonayo bungeni unaweza kuishinikiza serikali itekeleze matakwa ya waandamanaji.

Harakati hizo zinaonyesha kwamba maandamano nchini Iraq yanachochewa na kuongozwa na mitandao ya kijamii pamoja na mitandao ya vyombo vya habari vya maadui wa nchi hiyo; na kwa bahati mbaya, baadhi ya mirengo kama ule wa Sadr umenasa kwenye mtego wa mitandao hiyo bila kujitambua.

Kuhusiana na suala hilo, kanali ya televisheni ya Marekani ya Al-Hurrah imedai kuwa, harakati ya Al-Hashdu-Sha'abi na kamanda wa kitengo cha masuala ya usalama cha harakati hiyo vilikuwa na taksiri katika ufyatuaji risasi uliolenga waandamanaji. Mhandisi Nasr Ash-Shamri, msemaji wa harakati ya An-Nujabaa amejibu madai hayo kwa kusema: "Televisheni ya Al-Hurrah ya Marekani inazusha fitna na kuchochea mfarakano unaolenga mihimili ya wananchi wa Iraq; mfano wa karibuni kabisa ukiwa ni tuhuma zake dhidi ya Al-Hashdu-Sha'abi na kamanda wa kitengo chake cha usalama."

Nukta ya nne, ni kuhusu safari iliyofanywa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Mark Esper huko mjini Baghdad na mazungumzo aliyofanya na Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Ulinzi wa Iraq. Malengo ya safari ya Esper hayakutangazwa, lakini kabla ya safari hiyo, ubalozi wa Marekani mjini Baghdad ulikuwa umewekwa katika hali ya tahadhari. Ni wazi kwamba serikali ya Marekani haipendezwi na misimamo huru inayochukua serikali ya Iraq katika siasa zake za nje.

Kutoka kushoto: Rais Barham Salih, Spika wa Bunge Muhammad al-Halbousi na Waziri Mkuu Adil Abdul-Mahdi

Na nukta ya tano ni kuhusu kikao cha siku ya Jumatano kilichofanyika kwa uwenyekiti wa Rais Barham Salih na kuhudhuriwa na waziri Mkuu, Spika wa Bunge na Mkuu wa Vyombo vya Mahakama, ambapo viongozi hao walisisitiza kwamba watafuatilia matakwa ya wananchi na kulinda usalama na maisha ya waandamanaji. Adil Abdul-Mahdi alieleza pia katika kikao hicho kwamba anayasikia matakwa yanayopiganiwa na wananchi.

Lakini nukta ya kumalizia hapa ni kwamba, wakati wakuu wa mihimili mitatu ya dola wanasisitizia azma ya kutekeleza mageuzi ya kiuchumi na kuyafanyia kazi matakawa ya wananchi, ni muhimu Wairaqi wakaelewa kwamba, kuendeleza maandamano yanayochanganyika na ghasia na machafuko si tu hakuwezi kukidhi maslahi yao, lakini pia yataifanya hali ya mambo nchini humo iwe tete na tata zaidi.../