Pande zote nchini Yemen zatakiwa kuheshimu makubaliano ya Stockholm
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i57176-pande_zote_nchini_yemen_zatakiwa_kuheshimu_makubaliano_ya_stockholm
Mkuu wa Timu ya Wasimamizi wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen amesisitizia udharura wa pande zote nchini Yemen kuheshimu makubaliano ya Stockholm, Sweden.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 10, 2019 08:44 UTC
  • Pande zote nchini Yemen zatakiwa kuheshimu makubaliano ya Stockholm

Mkuu wa Timu ya Wasimamizi wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen amesisitizia udharura wa pande zote nchini Yemen kuheshimu makubaliano ya Stockholm, Sweden.

Abhijit Guha amezitaka pande zote nchini Yemen kuonyesha nia yao njema kwa kuheshimu makubaliano ya usitishaji vita ya Stockholm Sweden na kujiepusha na hatua yoyote ile ambayo inakiuka makubaliano hayo.

Mkuu wa Timu ya Wasimamizi wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen amebainisha kwamba, kuna udharura kwa pande zote nchini Yemen kuheshimu makubaliano hayo ya Stpckholm ambayo ni hatua moja mbele ya kuelekea katika kuyapatia ufumbuzi matatizo ya Yemen.

Makubaliano ya usitishaji vita ya Stockholm kati ya ujumbe wa Riyadh na Sana'a kuhusiana na Al-Hudaydah, yalianza kutekelezwa tarehe 18 Disemba mwaka jana, ingawa hata hivyo muungano vamizi wa Saudia umekuwa ukiyakiuka kila siku. Bandari ya Al-Hudaydah, ndio njia kuu ya kupitishia misaada ya kibinaadamu kwa ajili ya Yemen.

Yemen inavyoharibiwa vibaya na mashambulio ya anga ya Saudi Arabia na washirika wake

Saudi Arabia ikishirikiana na Marekani, Imarati, utawala haramu wa Israel  na nchi nyingine kadhaa ilianzisha mashambulizi makali dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 sambamba na kuizingira nchi hiyo ya Kiarabu katika pande tatu za nchi kavu, angani na baharini.

Hadi sasa vita hivyo vimepelekea watu laki moja kuuawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa. Vilevile mamilioni ya Wayemen wamelazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.