Watoto wa Kipalestina, wahanga wa jinai za utawala haramu wa Israel
(last modified Fri, 22 Nov 2019 07:07:30 GMT )
Nov 22, 2019 07:07 UTC
  • Watoto wa Kipalestina, wahanga wa jinai za utawala haramu wa Israel

Kituo cha kutetea haki za wafungwa wa Kipalestina cha "Palestinian Prisoners Club" kilitangaza katika maadhimisho ya Siku ya Watoto Duniani iliyoadhimishwa tarehe 20 Novemba katika maeneo mbalimbali duniani kwamba, watoto 745 wa Kipalestina wametiwa mbaroni tangu ulipoanza mwaka huu wa 2019 hadi kufikia mwezi uliopita wa Oktoba.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unaoua watoto, umekuwa hauuiti kutenda jinai yoyote ile dhidi ya Wapalestina. Watoto wa Kipalestina nao hawajasalimika na jinai zinazofanywa kwa mpangilio na utawala ghasibu wa Israel. Watoto wa Kipalestina siyo tu kwamba, wamekuwa wakishuhudia kwa macho yao kuuawa shahidi au kujeruhiwa wazazi wao, bali wao pia wamekuwa wakilengwa moja kwa moja na jinai za Israel.

Kuuawa shahidi, kujeruhiwa, kutiwa mbaroni, kupigwa, kudhalilishwa, kushtakiwa katika mahakama za kijeshi, kukabiliwa na vitisho mbalimbali pamoja na mashinikizo ni miongoni mwa jinai ambazo zimekuwa zikifanywa mchana kweupe na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina.

Tangu mwaka 2000 kulipoanza Intifadha ya Pili hadi sasa, zaidi ya watoto 2070 wa Kipalestina wameuawa shahidi na wanajeshi wa Israel wakishirikiana na walowezi wa Kizayuni. Watoto 50 wa Kipalestina waliuawa shahidi mwaka jana pekee.

Muhammad al-Durrah, mtoto wa miaka 12 wa Kipalestina alipouawa shahidi kwa kupigwa risasi akiwa amejificha nyuma ya baba yake

Aidha watoto 16 wa Kipalestina wameuawa shahidi katika miezi sita ya awali katika mwaka huu wa 2019 tena kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel. Takwimu zinaonyyesha kuwa, kwa akali watoto 46 wa Kipalestina wameuawa shahidi tangu yalipoanza maandamano ya 'Haki ya Kurejea" mwezi Machi mwaka jana.

Hapana shaka kuwa, moja ya taswira chungu kabisa na ya kusikitisha ya jinai za Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina ni ile iliyotokea Oktoba 2000 wakati Muhammad al-Durrah, mtoto wa miaka 12 wa Kipalestina alipouawa shahidi kwa kupigwa risasi akiwa amejificha nyuma ya baba yake na picha ya tukio hilo kuonyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni. Jinai hii ya Israel dhidi ya Muuhammad Durrah iligeuka na kuwa nembo ya muqawama na siku ya watoto wa Kipalestina wasio na hatia.

Kuwajeruhi watoto wa Kipalestina ni upande mwingine wa jinai za wanajeshi wa Israel. Kituo cha Utafiti na Utengenezaji wa Filamu za Matukio ya Kweli cha Kamati ya Masuala ya Wafungwa na Wapalestina Walioachiliwa Huru kimetangaza kuwa, kuanzia mwaka 1967 hadi sasa, utawala bandia wa Israel umewatia mbaroni zaidi ya watoto 50,000 wa Kipalestina, Watoto 1,233 wa Kipalestina walijeruhiwa kwa risasi na wanajeshi wa Israel katika miezi sita ya awali ya mwaka huu. Aidha tangu kuanza maandamano ya Haki ya Kurejea hadi sasa, zaidi ya watoto 2,000 wa Kipalestina wamejeruhiwa.

Kuwatia mbaroni na kuwashtaki katika mahakama za kijeshi watoto wa Kipalestina, ni upande mwingine pia wa jinai zinazofanywa na utawala wa Israel unaoua watoto.

Tangu kuanza mwaka huu hadi sasa watoto 745 wa Kipalestina wametiwa mbaroni. Nukta muhimu ni hii kwamba, utawala wa Israel umekuwa ukiwafungulia mashtaka watoto wa Kipalestina katika mahakama za kijeshi ambapo kwa mwaka watoto kati ya 500 hadi 700 wa Kipalestina hushtakiwa na kuhumiwa katika mahakama za kijeshi za utawala huo haramu. Kwa sasa, kuna takribani watoto 350 katika magereza ya Israel wakihudumia vifungo vyao.

Fauka ya hayo, mbali na jinai hizi za kuhusika zinazofanywa dhidi ya watoto wa Kipalestina, watoto hao wanakabiliwa na jinai zisizo za kuhisika kama vile mzingiro wa kila upande dhidi ya Ukanda wa Gaza ambao umekuwa na taathira hasi kama magonjwa, umasikini na njaa kwa wakazi wa eneo hilo wakiwemo watoto wadogo.

Watoto wa Kipalestina wakiwa korokoroni

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kutenda jinai dhidi ya watoto wa Kipalestina katika hali ambayo, kwa mujibu wa kipengee cha 16 cha hati ya haki za watoto, vitendo vya ukatili na utumiaji mabavu dhidi ya watoto vimepigwa marufuku.

Kile ambacho kinafanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina hatuwezi kukiita kama ni kitendo cha kutumia mabavu dhidi ya watoto bali ni 'jinai dhidi yya binadamu ambazo zinafanyika chini ya kimya cha jamii ya kimataifa na uungaji mkono wa moja kwa moja wa serikali ya Marekani, ambapo uungaji mkono huo umeongezeka zaidi katika kipindi cha serikali ya Rais Donald Trump.