Nov 24, 2019 11:33 UTC
  • Mahmoud Abbas: Dhulma ya Marekani haitodumu

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameonyesha kukasirishwa sana na uungaji mkono wa Marekani kwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi wanazoporwa Wapalestina na kusisitiza kuwa, dhulma ya Marekani haitodumu.

Itakumbukwa kuwa, Jumatatu ya wiki iliyopita, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alitangaza kuwa serikali ya Donald Trump imebadilisha siasa zilizochukuliwa na Barack Obama, rais wa zamani wa Marekani kuhusu ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Alisema, matamko ya kiserikali ya Marekani kuhusu ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hayakuwa na utaratibu mzuri na kusisitiza kuwa, Washington inaamini kwamba ujenzi wa vitongoji vya Israel katika ardhi za Wapalestina haukinzani na sheria yoyote ya kimataifa.

Marekani imetangaza waziwazi kuunga mkono jinai za Israel za kuwaga damu za Wapaletina, kuwapora ardhi zao na kujenga mahala pake vitongoji kama hivi vya walowezi wa Kizayuni

 

 

Shirika la habari la Palestina limemnukuu Mahmoud Abbas akijibu kwa hasira matamshi hayo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akisema kuwa, wananchi wa Palestina kamwe hawawezi kukubaliana na maamuzi hayo ya serikali ya Washington kama ambavyo hawakukubaliana pia na maamuzi ya huko nyuma ya Marekani.

Rais huyo wa Mamlaka ya Ndani ya Palesitna ameongeza kuwa, Quds ndio mji mkuu wa milele wa Palestina ambao hivi sasa unakaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni na kwamba makubaliano yote ya huko nyuma na Israel, yote yamesisitiza kuwa mji wa Baytul Muqaddas unakaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Hivi sasa kuna walowezi laki nne wa Kizayuni wanaishi kwenye vitongoji vya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na laki mbili wengine wako katika vitongoji vya Kizayuni vya Quds Mashariki. Sheria zote za kimataifa zinasisitiza kuwa, walowezi wote hao ni wavamizi na wanakaa kinyume cha sheria kwenye maeneo hayo.

Tags