Adel Abdulmahdi: Kile kinachoendelea kujiri huko Iraq ni fitna kubwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i57533-adel_abdulmahdi_kile_kinachoendelea_kujiri_huko_iraq_ni_fitna_kubwa
Waziri Mkuu wa Iraq amesisitiza kuwa kile kinachoendelea nchini humo hivi sasa ni fitna kubwa na kueleza kuwa serikali inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwaunga mkono wananchi licha ya mashinikizo chungu nzima.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 27, 2019 10:41 UTC
  • Adel Abdulmahdi: Kile kinachoendelea kujiri huko Iraq ni fitna kubwa

Waziri Mkuu wa Iraq amesisitiza kuwa kile kinachoendelea nchini humo hivi sasa ni fitna kubwa na kueleza kuwa serikali inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwaunga mkono wananchi licha ya mashinikizo chungu nzima.

Waziri Mkuu wa Iraq Adel Abdulmahdi leo Jumatano amekutana na baraza lake la mawaziri kujadili maandamano yanayoendelea nchini humo na namna ya kuamiliana na wafanya maandamano na kueleza kuwa: Vikosi vya usalama vinasisitiza kuwaunga mkono wafanya maandamano katika maidani wanapokutania. 

Abdulmahdi amesema kuwa baadhi ya ghasia zimetekelezwa na watu wasiojulikana na wanaovalia maski na kuongeza kuwa: Matukio ya kusikitisha yamejiri maandamanoni; na kamati ya uchunguzi imeweka wazi masuala hayo katika ripoti yake iliyowasilisha. 

Maandamano ya Iraq na uchomaji wa maeneo ya umma

Waziri Mkuu wa Iraq ameashiria nafasi ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo katika kulinda usalama wa nchi na kueleza kuwa serikali haiwezi kukaa kimya mbele ya hujuma zilizofanywa nchini humo kama uchomaji wa maeneo ya umma na kuibua ghasia na machafuko; la sivyo serikali itaanguka.

Wimbi la pili la maandamano lilianza katika maeneo mbalimbali nchini Iraq tangu Oktoba 25 mwaka huu na yangali yanaendelea hadi sasa. Wizara ya Ulinzi ya Iraq Jumapili wiki hii ilitangaza kuwa upande wa tatu unahusika katika mauaji na kuwashambulia waandamanaji na vikosi vya usalama kwa lengo la kuibua machafuko na migawanyiko huko Iraq.