Misri yatoa wito wa kuundwa nchi huru ya Palestina
(last modified Thu, 05 Dec 2019 10:26:36 GMT )
Dec 05, 2019 10:26 UTC
  • Misri yatoa wito wa kuundwa nchi huru ya Palestina

Mwakilishi wa kudumu wa Misri katika Umoja wa Mataifa ametilia mkazo udharura wa kuundwa nchi huru ya Palestina na kusema kuwa, amani na utulivu haviwezi kupatikana bila ya kuchukuliwa hatua hiyo.

Mohamed Idris amekiambia kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York kwamba, kadhia ya Palestina haiwezi kutatuliwa bila na kuundwa nchi huru ya Palestina. 

Idris amesema kuwa, haiwezekani kuzungumzia amani na usalama katika eneo la magharibi mwa Asia bila ya kupatikana ufumbuzi wa kiadilifu, wa pande zote na endelevu wa kadhia ya Palestina kupitia njia ya kuunda nchi ya Palestina katika mipaka ya tarehe 4 Juni mwaka 1967. 

Mwakilishi wa Misri katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, kadhia ya Palestina umebakia hivihivi bila ya kupatiwa ufumbuzi licha ya kupita miongo 7 sasa tangu ulipoundwa utawala wa Kizayuni wa Israel na hakuna upeo na mwangaza wa utatuzi wa kisiasa wa mgogoro huo.

Jumanne iliyopita pia viongozi wa harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina za Jihad Islami na Hamas walikutana mjini Cairo kujadili kadhia ya Palestina hususan mpango wa kishetani wa Marekani uliopewa jina la "Muamala wa Karne" kuhusu Palestina.

Mpango huo unaipa Israel mji mtakatifu wa Quds na kuwazuia wakimbizi wa Palestina walioimbilia nje kurejea katika nchi na makazi yao yaliyoghusubiwa na Wazayuni wa Israel.    

Tags