Kupasishwa sheria za uchaguzi nchini Iraq; hatua moja kuelekea mbele
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58112-kupasishwa_sheria_za_uchaguzi_nchini_iraq_hatua_moja_kuelekea_mbele
Jumanne ya tarehe 24 Disemba, Bunge la Iraq lilipasisha sheria mpya za uchaguzi nchini humo ambazo ni majumui ya vipengee 50.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 26, 2019 03:37 UTC
  • Kupasishwa sheria za uchaguzi nchini Iraq; hatua moja kuelekea mbele

Jumanne ya tarehe 24 Disemba, Bunge la Iraq lilipasisha sheria mpya za uchaguzi nchini humo ambazo ni majumui ya vipengee 50.

Kufanyiwa mabadiliko sheria za uchaguzi, kuweko marekebisho ya katiba, kuuzuliwa Waziri Mkuu na kuundwa serikali mpya ndio yaliyokuwa matakwa ya wananchi wa Iraq waliokuwa wakiandamana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.

Baada ya Waziri Mkuu Adil Abdul-Mahdi kujizulu, kuteuliwa wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi ni moja ya matakwa ya waandamanaji nchini Iraq ambayo yametekelezwa baada ya kupasishwa sheria mpya za uchaguzi nchini humo.

Kanuni za zamani za uchaguzi ni miongoni mwa sheria ambazo ziliandaliwa na kupasishwa na Wamarekani kwa ajiili ya Wairaq. Sheria hizi mpya za uchaguzi nchini Iraq zina tofauti mbili za kimsingi na sheria za hapo kabla za uchaguzi.

Tofauti ya kwanza ni kwamba, katika sheria za zamani wapiga kura walikuwa wakipigia kura orodha ya uchaguzi ya vyama, lakini katika sheria mpya za sasa, wapigaura badala ya kuipigia kura orodha ya uchaguzi ya vyama wanalazimika kuwapigia kura watu.

Wabunge wa Iraq wakipiga kura kupasisha sheria mpya za uchaguzi

Hali hii mbali na kupunguza uwajibikaji na mfungamano wa watu kwa vyama, ni sababu ya mabadiliko kwani kwa akali inapunguza ile hali ya mtazamo wa kikaumu na kihisa kwa siasa za utawala nchini Iraq.

Ukweli wa mambo ni kuwa, sheria mpya za uchaguzi nchini Iraq zinazingatia mgombea na hazizingatii chama. Sayyid Muqtada Sadr, Kiongozi wa Harakati ya Sadr amekaribisha kwa mikono miwili kupasishwa sheria hizo mpya na kusema kuwa, moja ya matakwa mengine ya wananchi wa Iraq yametekelezwa.

Tofauti ya pili ni hii kkwamba, kwa mujibu wa kipengee cha 15 cha sheria mpya, kila Mbunge atawakilisha jimbo moja tu la uchaguzi, na hali hii itahitimisha mwenendeo wa hapo kabla wa makundi ya uchaguzi kuwa wawakilishi wa mikoa yote.

Rais Barham Salih wa Iraq

Kimsingi ni kuwa, katika sheria mpya za uchaguzi, kila jimbo la uchaguzi litakuwa na mwakilishi wake Bungeni. Mabadiliko haya yanamfanya Mbunge kuwajibika na kuzingatia majukumu yake zaidi katika jimbo lake la uchaguzi  analoliwakilisha kinyume kabisa na hapo kabla.

Kipengee hiki cha sheria ya uchaguzi kilizua mizozo na malalamiko ya baadhi ya makundi na hivyo kupelekea upasishwaji wake uchelewe. Pamoja na hayo yote, lakini sheria mpya za uchaguzii nchini Iraq hususan kipengee kinachohusiana na majimbo ya uchaguzi, juzi Jumanne kililalamikiwa pia na Wakurdi na baadhi ya makundi ya Kisuni na hata baadhi ya jamii za waliowachache ambazo ziliamua kususia upigaji kura huo. Hata hivyo Bunge lilikamilisha akidi kwa ajili ya upigaji kura.

Upinzani huu unaonyesha kuwa, baadhi ya makundi na mirengo nchini Iraq ingali ina mitazamo na fikra za kimakundi na ugavi wa hisa ya uongozi.

Hii ni katika hali ambayo, kuhitimishwa mielekeo ya kimakundi na kihisa, ni moja ya matakwa ya maandamano ya wananchi wa nchi hiyo yaliyoanza tarehe Mosi Oktoba mwaka huu na ambayo yangali yanaendelea kwa uingiliaji wa madola ajinabi.

Adil-Abdul-Mahdi, aliyekuwa Waziri Mkuu  wa Iraq aliyejiuzulu  mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba

Kwa hakika kupasishwa sheria mpya za uchaguzi nchini Iraq inahesabiwa kuwa ni kupiga hatua moja mbele. Wakati huo huo, Muhammad al-Halbousi, Spika wa Bunge la Iraq siku ya Jumanne aliutambulisha kwa Rais Barham Salih mrengo wa al-Binaa kuwa ndio mrengo mkuu Bungeni.

Filhali, mrengo wa al-Bainaa unapaswa kuarifisha jina la mgombea wake wa nafasi ya Waziri Mkuu, ili azibe pengo lililoachwa wazi na Adil Abdul-Mahdi ambaye ombi lake la kujiuzuluu lilikubaliwa na Bunge tarehe Mosi mwezi huu.  Inapaswa kusubiri na kuona je, mirengo ya kisiasa nchini Iraq itaruhusu kuarifishwa Waziri Mkuu kupitia njia ya Bunge, au itapanda mawimbi ya medani ya Tahrir na mienendo ya wananchi?.