Netanyahu: Israel kusaini 'makubaliano ya amani' na nchi za Kiarabu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i58197-netanyahu_israel_kusaini_'makubaliano_ya_amani'_na_nchi_za_kiarabu
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesema Tel Aviv karibuni hivi itasaini makubaliano ya amani na kuufanya wa kawaida uhusiano wake na nchi kadhaa za Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 30, 2019 07:31 UTC
  • Netanyahu: Israel kusaini 'makubaliano ya amani' na nchi za Kiarabu

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesema Tel Aviv karibuni hivi itasaini makubaliano ya amani na kuufanya wa kawaida uhusiano wake na nchi kadhaa za Kiarabu.

Benjamin Netanyahu alisema hayo jana usiku na kuongeza kuwa, "Nina azma ya kukamilisha mchakato wa kufanya uhusiano wa Israel na nchi kadhaa za Kiarabu kuwa wa kawaida, na kusaini makubaliano ya amani ndani miaka michache ijayo."

Netanyahu amesema hayo katika hafla ya chama chake cha Likud jijini Tel Aviv ambapo amebainisha kwamba, kuwa na uhusiano wa kawaida na nchi za Kiarabu ni moja ya mafanikio yake makubwa ya kidiplomasia.

Katika hafla hiyo ya chama cha Likud, Netanyahu ameashiria juu ya safari yake nchini Oman, licha ya kuwa Tel Aviv na Muscat hazina uhusiano wa kidiplomasia.

Netanyahu na Sultan Qaboos mjini Muscat

Oktoba mwaka jana, Sultan Qaboos bin Said Al Said wa Oman alimpokea Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni Benjamin Netanyahu katika anga ya hofu iliyopo kwamba nchi kadhaa za Kiarabu zikiongozwa na Saudi Arabia na Imarati zinataka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu.

Jordan na Misri ndizo nchi mbili tu za Kiarabu zenye uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel, ingawaje nchi nyingine za Kiarabu zimekuwa na uhusiano wa kificho na utawala huo pandikizi.