Jan 28, 2020 11:58 UTC
  • Dakta Ali Larijani
    Dakta Ali Larijani

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema madhumuni ya njama za Marekani dhidi ya Wapalestina kwa jina la 'Muamala wa Karne' ni kuwadhalilisha na kuwatweza Waislamu.

Akihutubia kikao rasmi cha Bunge la Iran mapema leo, Dakta Ali Larijani amesema Marekani imepata uthubutu wa kuzindua njama zake hizo batili kutokana na mgawanyiko ulioko miongoni mwa Waislamu.

Huku akiashiria maandamano ya wananchi wa Iraq dhidi ya Marekani, Dakta Larijani amesema muda si mrefu Wamarekani wataelewa na kushuhudia matokeo ya njama zao hizo chafu zinazokusudia kuhalalisha jinai za Israel dhidi ya Wapalestina.

Wapalestina katika maandamano ya kupinga 'Muamala wa Kare'

Mpango wa Muamala wa Karne uliopendekezwa na Marekani unajumuisha kukabidhiwa kikamilifu Israel mji mtakatifu wa Quds wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa, vitongoji vilivyoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan vyote vipewe Israel na Wapalestina wasiwe na haki ya kurejea kwenye ardhi za mababu zao.

Mpango huo batili ambao Rais wa Marekani, Donald Trump anatazamiwa kuuzindua leo Jumanne mbele ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu umepingwa vikali na ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu na hata Wapalestina wenyewe.

Tags