Jeshi la Syria lakomboa maeneo mengine kaskazini mwa nchi hiyo
Jeshi la Syria huku likiendelea kusonga mbele upande wa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo limefanikiwa kuvikomboa vitongoji viwili huko kaskazini mwa mkoa wa Idlib ambavyo vilikuwa vikishikiliwa na magaidi wenye silaha.
Syria imefanikiwa kuvikomboa kikamilifu vitongoji vya Jubas na San huko kusini magharibi mwa Saraqib mashariki mwa mkoa wa Idlib. Jeshi hilo jana alasiri pia lilikikomboa kijiji kimoja kinachopatikana huko Khan Tuman magharibi mwa mji wa Halab kaskazini mwa Syria. Kijiji hicho kilikuwa chini ya udhibiti wa magaidi.
Jeshi la Syria siku kadhaa zilizopita lilianzisha oparesheni ya kijeshi kaskazini mwa nchi ikiwa ni jibu kwa hatua za magaidi za kukiuka mara kwa mara usitishaji vita katika mkoa wa Idlib. Hadi kufikia sasa jeshi la Syria limefanikiwa kudhibiti sehemukubwa ya mkoa huo. Mkoa wa Idlib ulikuwa ngome ya mwisho inayoshikliliwa na makundi ya kigaidi huko Syria; ambapo kwa kukombolewa mkoa huo na maeneo mengine huko magharibi mwa Halab na mashariki mwa Latakiya; kuwepo kwa ugaidi nchini humo kutahitimishwa.