Saudia yaitaka Ujerumani iendelee kurundika silaha nchini humo
Utawala wa Aal-Saud ambao unaendelea kumwaga damu za Wayemen umeiomba Ujerumani iondoe katazo la kutuma silaha nchini Saudi Arabia.
Katika mahojiano na shirika la habari la Ujerumani la DPA jana Jumatatu, Faisal bin Farhan Aal Saud, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia alidai utawala wa Riyadh unahitaji silaha hizo kwa ajili ya kujilinda.
Bin Farhan ameashiria kuhusu mashambulizi ya mwaka jana ya harakati ya Ansarullah ya Yemen dhidi ya vituo viwili vikubwa vya mafuta nchini Saudia na kudai kuwa, "Natumai Ujerumani inafahamu umuhimu wa silaha hizo kwa ajili ya kulilinda taifa letu."
Ombi la Saudia kwa Ujerumani linakuja wiki sita kabla ya Ujerumani kutafakari iwapo itarefusha muda wa kusitisha mauzo ya silaha kwa Saudia na karibu waitifaki wenzake wote wanaoshiriki katika jinai dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Yemen au la.
Marufuku ya Ujerumani ya kuizuia silaha Saudia inatazamiwa kumalizika Machi 31 mwaka huu. Ujerumani ilisitisha mauzo ya silaha zake kwa watawala wa Riyadh mwishoni mwa mwaka 2018, kufuatia mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji wa utawala wa Aal- Saud ndani ya ubalozi wa Saudia nchini Uturuki.
Ukoo wa Aal Saud na wavamizi wenzake wa Yemen wanatumia silaha za nchi za Magharibi kufanya jinai za kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wa Yemen.