Kumalizika mwaka wa tisa wa vita vya Syria
Leo Jumanne ya tarehe 16 Machi 2020, vita baina ya mfumo wa utawala wa Syria na makundi ya magaidi wanaotoka mataifa kadhaa duniani vimeingia katika mwaka wa kumi.
Maandamano ya kupinga serikali yalianza nchini Syria tarehe 15 Machi 2011 kwa sura ya kufuata mkumbo wa yale yaliyokuwa yakijiri katika nchi zingine za Kiarabu. Hata hivyo tofauti kubwa zaidi kati ya matukio ya Syria na yaliyotokea katika nchi nyingine za Kiarabu ni kwamba, malalamiko ya upinzani wa ndani nchini Syria yaligeuka kuwa vita kati ya mfumo wa utawala wa nchi hiyo na makundi ya kigaidi, kutokana na uingiliaji wa mhimili wa pande nne za Wamagharibi, Waarabu, Waebrania na Waturuki. Uingiliaji huo ulibadilisha sura ya matukio ya Syria yaliyokuwa ya upinzani wa amani wa ndani, na kuwa ya machafuko na umwagaji damu uliohusisha makundi ya magaidi kutoka zaidi ya nchi 80 duniani. Matokeo yake, na kinyume ilivyokuwa katika nchi zingine za Kiarabu, katika matukio ya Syria mfumo wa utawala wa nchi hiyo haukukabiliana na upinzani wa raia wake, bali ulipambana na watu waliolipwa fedha na nchi zingine ili kuanzisha vita dhidi ya mfumo huo.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Syria yametoa ripoti mpya ya takwimu za waathirika wa vita hivyo vya ndani na kutangaza kuwa, watu wasiopungua laki tatu na 84 elfu wameuawa katika kipindi cha miaka tisa iliyopita, mamia ya maelfu wamejeruhiwa, na wengine wapatao milioni 12 wamepoteza makazi yao na kulazimika kuwa wakimbizi. Ijapkuwa lengo la vita hivyo vya kigaidi lilikuwa ni kuuangusha mfumo wa utawala wa Syria na hata kuigawanya vipande vipande nchi hiyo, lakini malengo hayo hayajaweza kufikiwa; na badala yake wananchi wa Syria wamekuwa wahanga na waathirika wakubwa zaidi wa vita vilivyoendeshwa dhidi yao kwa uungaji mkono wa hali na mali wa wanaojigamba kuwa ni watetezi wa demokrasia na haki za binadamu. Geir Pedersen, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria amelielezea hilo kwa kusema: "Adhabu na mateso waliyohimili wananchi wa Syria katika muongo huu wa kutisha na kuhuzunisha hayakadiriki wala hayatasawariki."
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, nalo pia lilitoa ripoti hivi karibuni kwa mnasaba wa kumalizika mwaka wa tisa wa vita vya ndani nchini Syria na kutangaza kuwa "matokeo ya vita vya Syria yamekuwa ni kushuhudia mtoto mmoja akiaga dunia katika kila muda wa masaa kumi." Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na UNICEF tarehe 9 Machi, tangu mwaka 2014 hadi 2019, idadi ya watoto waliouawa kutokana na vita vya Syria imefikia 5,427. Wataalamu wamekadiria pia kuwa, watoto zaidi ya milioni tano walioko ndani ya Syria na wengine wapato milioni mbili na nusu waliokimbiuliza nchi jirani wanahitaji msaada. Lakini mbali na hayo, karibu asilimia 80 ya watu waliosalia nchini Syria wanaishi chini ya mstari wa umasikini.
Mwaka wa tisa wa vita vya Syria umemalizika huku jeshi la nchi hiyo likiwa linatamba kwenye medani za vita, katika awamu ya mwisho ya operesheni za kupambana na ugaidi, za kuyakomboa maeneo yaliyosalia ya mkoa wa Idlib kutoka kwenye makucha ya magenge ya kigaidi. Mkoa huo ambao tangu mwaka 2015 umekuwa ukikaliwa kwa mabavu na kundi la Tahriru-Sham, ambalo ni genge la zamani la kigaidi la Jabhatu-Nusrah, unahesabiwa kuwa ngome ya mwisho ya wapinzani wa serikali ya Rais Bashar al-Assad.
Wakati jeshi la Syria lilipokuwa eneo la kilomita saba la mji wa Idlib, ambao ni makao makuu ya Mkoa wa Idlib, jeshi la Uturuki lilishambulia ngome zake ili kuzuia kukamilika ushindi wa jeshi hilo. Mhimili wa Magharibi unaoongozwa na Marekani ambao umekiri kuwa umeshindwa kumng'oa madarakani Rais Bashar al-Assad, sasa unaendeleza uafriti wa kukwamisha mchakato wa kisiasa sambamba na kuchochea mfarakano wa ndani, hususan kati ya Wakurdi na mfumo wa utawala wa Syria. Nao mhimili wa Waarabu, ambao umesalimu amri na kuungama kuwa umeshindwa kufikia malengo yake nchini Syria, hivi sasa unawaza na kuwazua jinsi ya kuirejesha nchi hiyo katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.
Inavyoonekana, mwaka wa kumi wa vita vya Syria unaweza ukawa ndio mwaka wa kumalizika vita hivyo, sambamba na kuendelea uafriti wa Magharibi ikiongozwa na Marekani wa kukwamisha mchakato wa maridhiano ya kisiasa ya nchi hiyo.../