Kutangazwa Benny Gantz, mwisho au fursa kwa Benjamin Netanyahu?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59821-kutangazwa_benny_gantz_mwisho_au_fursa_kwa_benjamin_netanyahu
Reuven Rivlin, Rais wa Utawala Haramu wa Israel amemwamuru rasmi Benny Gantz, Kiongozi wa Muungano wa Blu na Nyeupe, kuunda serikali mpya ya Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 18, 2020 09:26 UTC
  • Kutangazwa Benny Gantz, mwisho au fursa kwa Benjamin Netanyahu?

Reuven Rivlin, Rais wa Utawala Haramu wa Israel amemwamuru rasmi Benny Gantz, Kiongozi wa Muungano wa Blu na Nyeupe, kuunda serikali mpya ya Israel.

Uchaguzi wa tatu wa Bunge la utawala haramu wa Israel katika kipindi cha mwaka mmoja wa uliopita, ulifanyika tarehe pili Machi mwaka huu. Matokeo ya uchaguzi huo yalionyesha kuwa, chama cha mrengo wa kulia cha Likud kinachoongozwa na Benjamin Netanyahu kiliibuka na ushindi mdogo. Kwa mujibu wa matokeo hayo, chama cha Likud kilipata viti 37 kati ya viti vyote 58 vya mrengo wa kulia katika bunge la Israel. Muungano wa Blu na Nyeupe unaoongozwa Benny Gantz ulipata viti 32 na hivyo kuufanya mrengo wa kushoto na ule wa kati kutimiza viti 40 ndani ya bunge la Israel. Makundi ya Kiarabu baada ya Likud na Mrengo wa Blu na Nyeupe, yamepata viti 15. Chama cha Yisrael Beiteinu kinachoongozwa na Avigdor Lieberman kimepata viti 7 vilivyosalia kati ya viti 120 vya bunge la utawala khabithi wa Israel Knesset. Ili chama kiweze kuunda serikali kinahitaji kupata viti 61 katika bunge. Vyama vya Kiarabu kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa Septemba 17 mwaka jana, vimetangaza kumuunga mkono Benny Gantz. Septemba mwaka jana mrengo wa Kiarabu uliokuwa na viti vitatu vya bunge wakati huo, haukuwa tayari kumuunga mkono Gantz, lakini hivi sasa vyama vyote vya Kiarabu vimetangaza uungaji mkono wao kwa kiongozi huyo.

Benjamin Netanyahu anayekabiliwa na hatma mbaya iwapo Gantz ataweza kuunda serikali

Suala hilo linaonyesha kwamba, makundi ya kiarabu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu yamepata nguvu kubwa zaidi katika muundo wa utawala. Makundi hayo ya Waarabu ambayo awali hayakuwa yakipewa umuhimu wowote katika muundo wa serikali ya Israel,  sasa yanahesabika kuwa wachezaji na turufu muhimu ndani ya Israel. Japokuwa uungaji mkono wa Warabu kwa Benny Gantz ndio uliomuwezesha kupewa kibali cha kuunda serikali mpya, lakini suala hilo pia ni moja ya changamoto kubwa kwa Gantz. Hii ni kwa kuwa chama cha mrengo wa kushoto cha Gesher kimetangaza kuwa hakitashiriki katika serikali ambayo inaungwa mkono na muungano wa makundi ya Kiarabu.

Ni baada ya uungaji mkono wa Warabu kwa Gantz na hatua ya Avigdor Lieberman kujitenga na Benjamin Netanyahu, sambamba na kuonesha nia ya uungaji mkono wake kwa Gantz, ndipo Rais wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Reuven Rivlin akamwamuru kiongozi huyo wa Muungano wa Blu na Nyeupe kuunda serikali mpya. Duru zinazofuatilia matukio ya Israel zinaeleza kuwa, sambamba na muungano wa Warabu, mrengo wa Avigdor Lieberman pia utakuwa kati ya turufu muhimu katika muundo wa serikali mpya ya utawala huo. Itakumbukwa kuwa Lieberman alihusika katika kusambaratika serikali ya Netanyahu hapo mwezi Novemba 2018, na baada ya chaguzi za Aprili na Septemba 2019 pia alikuwa na nafasi kuu katika kumkwamisha Netanyahu kwenye harakati zake za kuunda serikali mpya. Baada ya uchaguzi wa tarehe pili Machi mwaka huu pia Avigdor Lieberman alitangaza wazi kwamba, hatashiriki katika serikali ambayo waziri mkuu wake ana faili jeusi la ufisadi katika mahkama ya Israel.

Netanyahu ambaye katika kila uchaguzi ameshindwa kupata ushindi mutlaki

Nukta muhimu ya kuashiriwa hapa ni kwamba, mwezi Septemba mwaka uliopita na licha ya kwamba Muungano wa Blu na Nyeupe ulikuwa umepata viti vingi kuliko chama cha Likud, lakini Reuven Rivlin bado alimtaka Netanyahu ndiye aunde serikali mpya ya Israel; hata hivyo alishindwa kufanya hivyo. Hivi sasa Gantz ametakiwa kuunda serikali mpya huku chama cha Likud kinachoongozwa na Benjamin Netanyahu kikiwa na viti vingi bungeni kuliko Muungano wa Blu na Nyeupe. Kwa sababu hiyo, hata kama hivi sasa Gantz amepiga hatua moja mbele kuelekea kwenye uwaziri mkuu kuliko Netanyahu, lakini iwapo hatafanikiwa kuunda serikali mpya, basi kwa mara nyingine Netanyahu atatakiwa tena kuunda serikali ya Israel. Wakati huo kutokana na kwamba makundi mengi ya kisiasa hayapendelei kufanyika uchaguzi wa bunge wa kwa mara ya nne katika kipindi cha mwaka mmoja, hivyo uwezekano wa Benjamin Netanyahu kuunda serikali, utakuwa mkubwa zaidi.