Saudi Arabia yaendelea kuishambulia kijeshi Yemen na kufanya uharibifu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60157-saudi_arabia_yaendelea_kuishambulia_kijeshi_yemen_na_kufanya_uharibifu
Kanali ya Televisheni ya al-Masirah imetangaza kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya Yemen umeendelea kuishambulia kijeshi nchi hiyo na kutekeleza mashambulio 19 katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita,
(last modified 2026-08-14T10:24:44+00:00 )
Apr 04, 2020 03:16 UTC
  • Saudi Arabia yaendelea kuishambulia kijeshi Yemen na kufanya uharibifu

Kanali ya Televisheni ya al-Masirah imetangaza kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vya Yemen umeendelea kuishambulia kijeshi nchi hiyo na kutekeleza mashambulio 19 katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita,

Kwa mujibu wa Kanali ya Televisheni ya al-Masirah, miji iliyoandamwa na mashambulio ya vikosi vamizi vinavyoongozwa na Saudi Arabia katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita ni Sa'adah, Ma'rib, Imran na Hajjah.

Kwa akali watu watatu wanaripotiwa kupoteza maisha yao katika mashambulio hayo huku makumi ya wengine wakijeruhiwa.

Hivi karibuni kituo cha Haki za Binaadamu cha Ain Al-Insaniyah kilielezea kuuawa na kujeruhiwa zaidi ya Wayemen elfu 42 katika kipindi cha miaka sita ya uvamizi na mashambulizi ya muungano vamizi wa Saudia nchini Yemen.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya taasisi au miundombinu iliyoharibiwa nchini Yemen katika kipindi cha miaka sita ya uvamizi huo, imefikia 8,610 na kwamba mashambulizi ya muungano wa Saudia yamesababisha uharibifu kwenye viwanja vya ndege 15, bandari 16, vituo 297 vya kuzalisha umeme na vituo 520 vya mawasiliano.

Saudi Arabia ikipata uungaji mkono wa Marekani, Imarat, Israel na nchi nyingine za Magharibi, ilianzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 sambamba na kutekeleza mzingiro wa anga, nchi kavu na baharini dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.

Hata hivyo kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen, hadi sasa Saudi Arabia na waitifaki wake wameshindwa kufikia malengo yao haramu.