Maelfu waandamana Israel dhidi ya serikali ya mseto ya Netanyahu
Maelfu ya raia wa utawala haramu wa Israel wamefanya maandamano kupinga makubaliano ya kuunda serikali ya muungano baina ya Benjamin Netanyahu ambaye ni kiongozi wa chama cha Licud na kiongozi wa chama cha Blue and White, Benny Gantz, huku wakimtaja Waziri Mkuu huyo wa Israel kama mshukiwa wa jinai na kiongozi fisadi ambaye hapaswi kuendelea kuuongoza utawala huo bandia.
Wamesema kuachwa Netanyahu aendelee kuongoza chini ya makubaliano hayo katika hali ambayo angali ana ushawishi katika uteuzi wa majaji na maafisa wa mahakama, ni sawa kuinajisi demokrasia, na lengo kuu la kuruhusu hilo ni kumnusuru Netanyahu ili aondokane na jinamizi la kisheria linalomkodolea macho.
Waandamanaji hao katika mji mkuu Tel Aviv walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kumkashifu Netanyahu, baadhi ya mabango hayo yakimtaja mwanasiasa huyo kama 'Waziri wa Ufisadi' na 'Waziri wa Jinai.'
Jumatatu iliyopita, Netanyahu na kiongozi wa chama cha Blu na Nyeupe, Benny Gantz walisaini makubaliano ya kugawana madaraka, baada ya wiki kadhaa za mazungumzo bila tija.
Hatimaye wawili hao walikubaliana kuunda serikali ya mseto yenye masharti mengi baada ya mashinikizo ya ndani na nje ya utawala huo wa Kizayuni. Utawala huo haramu ulitumbukia kwenye kinamasi hicho cha mkwamo wa kisiasa, baada ya kufanyika chaguzi tatu za bunge kwenye kipindi cha mwaka mmoja uliopita, bila chama chochote cha kisiasa kupata ushindi mutlaki wa kukiwezesha kuunda serikali.
Waziri Mkuu huyo wa utawala pandikizi wa Israel anatazamiwa kupandishwa kizimbani mwezi ujao, akikabiliwa na mashitaka ya ufisadi wa kifedha.