May 08, 2020 08:15 UTC
  • HAMAS na Jihadul Islami zapinga mpango wa kufanya mazungumzo na Israel

Harakati za Muqawama wa Kiislamu za Palestina HAMAS na Jihadul-Islami zimekosoa vikali mpango wa baadhi ya nchi za Kiarabu wa kutaka kurejea kwenye meza ya mazungumzo na utawala haramu wa Israel.

Afisa wa ngazi za juu wa Jihadul-Islami, Khaled Al-Batsh amesema mwaliko wa kufanya mazungumzo na utawala wa Kizayuni ni njama za kuepuka kukabiliana na adui na utumiaji wa vyombo visivyo na maana kurefusha ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina unaofanywa na utawala huo ghasibu.

Amesema kile ambacho kinahitajika kufanywa ni kujiondoa kwenye Mapatano ya Oslo yaliyofikiwa kati ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na utawala haramu wa Israel na wala si kurejea katika mazungumzo.

Naye Salah al-Bardawil, afisa mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS amesema kutaka kufanya mazungumzo na Israel kuna maana ya kuufanya wa kawaida uhusiano na utawala huo bandia na kwamba Wapalestina hawataruhusiwa kuzungumzia ardhi na haki zao kwenye mazungumzo hayo.

Baadhi ya Waarabu wanafanya juu chini kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel 

Ameeleza bayana kuwa, hatua yoyote ile ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel katu haikubaliki kwani inakwenda kinyume kabisa na maslahi ya wananchi wa Palestina.

HAMAS imekuwa ikisisitiza kuwa, ili kukabiliana na hatua na mienendo mibaya ya utawala ghasibu wa Israel, kuna haja ya kuweko umoja, mshikamano pamoja na uratibu katika umma wa Kiislamu na kuwatimua watu ambao wanafuatilia suala la kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo bandia.

Tags