Mwaka wa tatu wa mzozo baina ya nchi za Kiarabu
(last modified Fri, 05 Jun 2020 12:47:08 GMT )
Jun 05, 2020 12:47 UTC
  • Mwaka wa tatu wa mzozo baina ya nchi za Kiarabu

Ijumaa Juni tano 2020 imesadifiana na kuingia mwaka wa nne tangu uanze mgogoro baina ya nchi kadhaa za Kiarabu.

Saudi Arabia, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), nchi tatu ambazo ni wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, pamoja na Misri, mnamo Juni 5 mwaka 2017 ziliituhumu Qatar kuwa inaunga mkono ugaidi na zikakata uhusiano wao na nchi hiyo. Aidha nchi hizo nne zilifunga mipaka yao na Qatar baharini, angani na nchi kavu.

Mwaka wa tatu wa mvutano baina ya nchi hizo umemalizika ambapo nchi hizo nne, zinazoongozwa na Saudia, ambazo zimeizingira Qatar zimefeli katika sera zao za mzingiro. Qatar kwa upande wake  imeweza kuvuka changamoto za awali za mzingiro huo na sasa inaonekana kuzishinda nchi hizo nne mahasimu wake yaani Saudi Arabia, UAE, Bahrain na Misri.

Saudi Arabia na nchi hizo tatu zilitangaza masharti 13 ambayo Qatar ilipaswa kuyatimiza kabla ya uhusiano kurejea lakini Qatar imesema masharti hayo yanakiuka mamlaka yake ya kujitawala na imekataa kuyatekeleza.

Saudi Arabia inaamini kuwa  nchi zote za Ghuba ya Uajemi zinapaswa kuifuata katika sera zake sza kikanda na kimataifa lakini Qatar imepinga ubabe huo wa utawala wa ukoo wa Aal Saud. Hivi sasa baada ya miaka mitatu Qatar imeweza kuvuka vikwazo ilivyowekewa na hivyo imeweza kuifanya Saudia ielewe kuwa nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi zinajitegemea na zinatekeleza sera za kigeni zitakavyo.

Katika sera zake za vikwazo na mzingiro, Saudi Arabia imekuwa ikijaribu kuishinikiza Qatar ipunguze ushirikiano uliopo baina yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na Uturuki, hata hivyo kinyume na walivyotaraji wakuu wa Saudia, hivi sasa uhusiano wa Qatar na nchi hizo mbili umezidi kuimarika zaidi ya miaka ya nyuma.

Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani, Amir wa Qatar

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki ni nchi mbili muhimu ambazo zimeweza kuisaidia Qatar kufanikiwa kukabiliana na mzingiro na vikwazo. Kwa msingi huo wakuu wa Doha mbali na kukosoa vikali sera za Saudi Arabia wametangaza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki zinaheshimu uhuru wa nchi jirani na hazingilii mambo ya ndani ya nchi hizo.

Tokea mwanzo wa mgogoro baina ya nchi hizo tano za Kiarabu, serikali ya Marekani imekuwa ikionyesha misimamo kinzani. Mwanzoni mwa mgogoro huu, Rais Donald Trump alionyesha waziwazi kuipendelea Saudia na nchi zingine tatu lakini Rex Tillerson Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wakati huo alionekana kuunga mkono Qatar. Utawala wa Trump ulitumia mgogoro wa nchi hizo tano za Kiarabu, ambazo ni waitifaki wa Marekani, kuifaidisha nchi yake kiuchumi kupitia uuzaji silaha. Mwanzoni mwa mgogoro huo Marekani iliziuzia Saudia, UAE na Qatar idadi kubwa ya silaha kama vile ndege za kivita na makombora. Aidha mara kwa mara Trump alikuwa akiishinikiza Qatar na wakati mwingine pia aliishinikiza Saudia kupunguza mgogoro na uhasama baina yao. Lakini kilo ambacho Trump ameonyesha ni kuwa, kuendelea mgogoro baina ya nchi hizo za Kiarabu ni kwa maslahi yake.

Katika kipindi hiki cha kuanza mwaka wa nne wa mgogoro baina ya nchi tano za Kiarbau, baadhi ya duru zinadokeza kuwa, Donald Trump anazishinikiza Saudia na UAE kuondoa marufuku ya ndege za Qatari kuruka katika anga ya nchi zao. Pamoja na hayo, mashinikizo hayalengi kuhitimisha mgogoro huo bali sababu kuu ni kuwa, baada ya Qatar kuzingirwa na nchi nne za Kiarabu, ndege za Qatar zimekuwa zikitumia anga ya Iran zaidi ya miaka ya nyuma na kwa msingi huo Trump anataka kupunguza idadi ya ndege za Qatar zinazoruka katika anga ya Iran.

Mfalme Salman wa Saudia

Nukta ya mwisho hapa ni kuwa, katika  kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kumefanyika jitihada nyingi hasa na Kuwait kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro baina ya nchi hizo tano za Kiarabu. Lakini kutokana na sisitizo la Qatar la kuendelea kuwa na uhuru wa kujichukulia maamuzi yakwe yenyewe, na vilevile ulazima wa kuondolewa vikwazo na mzingiro, upatanishi huo wa Kuwait haujazaa matunda. Sasa wakati wa kuingia mwaka wa nne wa mzozo baina ya nchi hizo tano za Kiarabu, Sabah Al Khalid Al Sabah, Waziri Mkuu wa Kuwati, amesema Amiri wa Kuwait ataendeleza jitihada za kutatua mgogoro baina ya nchi hizo za Kiarabu. Pamoja na hayo bado hakuna dalili zozote kutoka Riyadh au Doha zinazoashiria azma ya kuhitimisa mgogoro huo.

Tags