Njama mpya nchini Lebanon; fitina za kimadhehebu kwa mbinu za kisiasa
Katika siku za karibuni Lebanon kwa mara nyingine imekuwa ikishuhudia machafuko ambapo watu wa kushukiwa na kutiliwa shaka wamekuwa wakimiminika mitaani na kupiga nara za kichochezi na za fitiza za kimadhehebu pamoja na kukabiliana na walinda amani nchini humo.
Tokea mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2019 Lebanon imekuwa ikishuhudia maandamano dhidi ya serikali ambayo yamepelekea kujiuzulu Saad Hariri kutoka kwenye kiti cha waziri mkuu na kiti hicho kukabidhiwa waziri mkuu mpya Hassan Diab mwezi Januari 2020. Katika kipindi cha chini ya miezi mitano tokea ashike usukani Hassan Diab, Lebanon imeshuhudia maandamano matatu makubwa dhidi ya serikali yake. Maandamano ya kwanza yalifanyika usiku wa siku ile ile ya Januari 21 ambapo Diab aliidhinishwa na bunge kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo. Duru ya pili ya maandamano hayo dhidi ya serikali ilifanyika mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu na ya tatu kuanzia Juni 6. Kuna maswali matatu muhimu kuhusu maandamano hayo ya Lebanon, la kwanza likini ni nini chanzo chake?
Wachambuzi wengi wanaamini kwamba maandamano ya hivi sasa dhidi ya serikali ya Diab hayana uhusiano wowote na yale yaliyofanyika dhidi ya Saad Hariri Oktoba mwaka jana. Hii ni kwa sababu maandamano hayo yalikuwa yanapinga hali mbaya ya kiuchumi ambapo waandamanaji walikuwa wakilalamikia hali mbaya ya kimaisha. Licha ya kuwa maandamano ya hivi sasa kidhahiri ni ya kiuchumi lakini chanzo chake hasa ni cha kisiasa.
Nara ambazo zimekuwa zikipigwa katika maandamano hayo dhidi ya Hizbullah ya Lebanon, ni moja ya sababu zinazoyafanya maandamano hayo kuwa ya kisiasa. Waandamanaji wanaituhumu Hizbullah kwa kueneza ufisadi nchini katika hali ambayo katika maandamano ya mwezi uliopita, walikuwa wakimtuhumu Riadh Salameh, Gavana wa Benki Kuu ya Lebanon na ambaye ni mmoja wa washirika wakubwa wa mrengo wa Machi 14, kwa kuhusika na ufisa na upunguzaji wa thamani ya sarafu ya nchi hiyo. Mwezi uliopita, Salameh alianza kutekeleza rasmi vikwazo mbalimbali vya Marekani, vikiwemo vya kifedha, dhidi ya Hizbullah kutokana na madai bandia ya Washington dhidi ya harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu.
Nara ambazo zimekuwa zikipigwa na waandamanaji hivi karibuni zinadhihirisha wazi kuwepo kwa mrengo ambao unachochea fitina za kimadhehebu nchini humo jambo ambalo limewapelekea viongozi rasmi wa nchi hiyo akiwemo Rais Michel Aoun na Spika Nabii Berri kutahadharisha dhidi ya jambo hilo. Rais Auon amesema kuwa matukio ya hivi karibuni nchini humo ni kengele ya hatari kwa Walebanon wote ili wasije wakatumbukia kwenye shimo refu la vita vya ndani. Naye Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon amesema: Matukio ya hivi karibuni ya Lebanon yanalenga umoja wa Walebanon wote.
Swali lingine ni kuwa je, ni nani anayechochea maandamano hayo?
Bada ya matukio ya mwishoni mwa mwezi Aprili na mwanzoni mwa mwezi Mei mwaka huu, Hassan Diab, Waziri Mkuu wa Lebanon, alizungumzia wazi kuwepo njama zinazofanywa na vibaraka wanaodhaminiwa kifedha na kisiasa na wageni kwa lengo la kuvuruga umoja wa nchi hiyo. Hivi sasa inaonekana wazi kwamba vibaraka hao wanaolipwa na utawala wa Kizayuni na Israel wanachochea hisia za kimadhehebu kwa shabaha ya kufikia malengo ya kisiasa yanayofuatiliwa na mabwana zao hao wa kigeni. Wapinzani wa Hizbullah ya Lebanon ambayo katika kipindi cha muongo mmoja wa karibuni imepata ushindi mkubwa katika medani ya mapambano dhidi ya ugaidi na vilevile kuibuka mshindi katika uchaguzi wa bunge wa 2018, wamekasirishwa sana na mafanikio ya kundi hilo la Kiislamu nchini Lebanon katika miaka ya karibuni, na hivyo wamekuwa wakifanya kila wanaloweza, yakiwemo maandamano ya kichochezi ili kulidhoofisha kisiasa kundi hilo.
Nukta ya mwisho ni kwamba harakati za karibuni nchini Lebanon, hata katika kipindi cha kupigiwa kura ya imani serikali ya Hassan Diab katika bunge, ambapo baadhi ya mirengo mashuhuri ya kisiasa ya nchi hiyo ilisusia kikao hicho, ni jambo lililotarajiwa. Katika kipindi cha nusu muongo uliopita serikali ya Lebanon imekuwa ikiongozwa na Saad Hariri na mrengo wake unaoungwa mkono na nchi za Magharibi na vibaraka wao katika eneo, ambao sasa ndio waibuaji wakubwa wa machafuko na maandamano yanayoendea katika nchi hiyo ya Kiarabu.