Harakati ya Jihad Islami ya Palestina yasisitiza kuendeleza mapambano
Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imesisitiza azma na irada yake ya kuendeleza jihadi na mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel
Katika taarifa, Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imetoa wito kwa umma wa Kiislamu duniani kuungana kwa ajili ya kukabiliana na adui Mzayuni. Harakati hiyo ya kupigania ukombozi wa Palestina imetoa wito kwa mataifa ya Kiislamu duniani kuweka kando hitilafu zao na kushirikiana ili kuweza kulisaidia taifa la Palestina.
Jihad Islami imewataka viongozi wote na maulamaa wa umma wa Kiislamu duniani kuweka hitilafu zao kando sambamba na kusitisha malumbano baina yao na kusaidia katika kuleta umoja miongoni mwa Wapalestina.
Aidha Jihad Islami imetahadharisa kuhusu baadhi ya nchi za Kiislamu na baadhi ya wale ambao wako mstari wa mbele katika kuleta uhusiano wa kawaida na adui Mzayuni na kuwataja watu kama hao kuwa ni wenye kuibua fitina na kuwasha moto wa vita.
Kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ni mpango ambao unatekelezwa katika fremu ya mapatnao ya 'muamala wa karne' ambayo ni mapatano ya kibaguzi yanayopigiwa debe na Marekani kwa lengo la kukandamiza kikamilifu haki za Palestina.
Mpango wa kidhulma wa "Muamala wa Karne" unasema kwamba mji wa Quds au Jerusalem wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu yaani Msikiti wa al Aqsa, ukabidhiwe utawala wa Kizayuni, wakimbizi wa Palestina wapokonywe haki yao ya kurejea kwenye ardhi zao, na Wapalestina wapewe vijipande vidogo vidogo tu vilivyotapakaa hapa na pale katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza.