Yemen yawasilisha mashtaka Umoja wa Mataifa dhidi ya Saudi Arabia
Spika wa Bunge la Yemen amesema kuwa uhalifu unaofanywa na Saudi Arabia na washirika wake nchini humo na kuendelezwa mzingiro wa nchi hiyo haviwezi kuhalalishwa kw njia yoyote ile.
Mohammed Hussein al-Aidarous amewatumia barua Katibu Mkuu wa Uumoja wa Mataifa, Antonio Guterres na mjumbe wa umoja huo katika masuala ya Yemen, Martin Griffiths na kueleza hali halisi kuhusu mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake huko Yemen na vilevile taathira za mashambulizi hayo kwa maisha ya raia wa nchi hiyo.
Hussein al-Aidarous amesema kuwa, uhalifu unaofanywa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen na hatua ya wavamizi hao ya kuzuia meli zinazobeba nishati na chakula kutia nanga katika bandari za Yemen ni jinai na uhalifu mkubwa ambao hauwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile.
Amesisitiza kuwa, mzingiro na vikwazo vya kidhalimu dhidi ya watu wa Yemen vinakwamisha jitihada za kupeleka chakula nchini humo na kuzidisha machungu na mashaka ya Wayemeni. Al-Aidarous ameongeza kuwa, kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya uhalifu huo kinazidisha mashaka na machungu hayo.
Spika wa Bunge la Yemen ameitaka jamii ya kimataifa kudumisha mashinikizo dhidi ya Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen kwa shabaha ya kukomesha mzingiro na kuruhusu shehena za meli zinazobeba mafuta, chakula na dawa kutia nanga katika bandari za Yemen.