OIC yavunja kimya chake kuhusu kuanzishwa uhusiano na Israel
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imesema nchi wanachama wake hazitafuata mkondo wa Umoja wa Falme za Kiarabu wa kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Kizayuni, hadi pale utawala huo ghasibu utakapoacha kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Katika taarifa ya jana Jumatatu, Katibu Mkuu wa OIC, Yusuf bin Ahmed al-Uthaymeen amesema ndoto ya kuufanya wa kawaida uhusiano na Israel katu haitafikiwa mpaka pale ukaliaji wa mabavu wa ardhi zote za Palestina ikiwemo mashariki mwa mji wa Quds wa tokea mwaka 1967 unaofanywa na Israel utakapofikia tamati, sambamba na kuundwa taifa huru la Palestina.
Amesema nchi zote wanachama wa OIC kwa kauli moja zimeafikiana juu ya kusitisha ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Palestina, na vile vile kuhakikisha Wapalestina wanapata haki zao za msingi.
OIC imesema siasa za ukandamizaji za utawala vamizi wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina zinatia wasiwasi mkubwa hasa vitendo vya utawala huo vya kubomoa nyumba za Wapalestina na kujenga vitongoji vipya vya walowezi wake; na mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza na maeneo mengine ya Palestina.
Agosti 13, pande mbili za Abu Dhabi na Tel Aviv zilisaini mkataba na kuafikiana rasmi kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia. Makubaliano hayo kati ya Israel na Imarati yamekabiliwa na wimbi kali la malalamiko na upinzani ndani na nje ya Palestina.