Wapalestina, Wabahrain walaani; Misri, UAE zakaribisha Bahrain kuanzisha uhusiano na Israel
Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu UAE zimekaribisha kuanzishwa uhusiano rasmi wa kidiplomasia kati ya Bahrain na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Rais Donald Trump wa Marekani usiku wa kuamkia leo alitangaza kuwa Bahrain na Israel zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina yao.
Jana hiyo hiyo usiku, Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri aliandika ujumbe kwenye ukurasa wa kijamii wa Twitter, wa kukaribisha mapatano yaliyofikiwa kati ya Bahrain na utawala wa Kizayuni na kudai kwamba, makubaliano hayo ni hatua muhimu kwa ajili ya amani katika Asia Magharibi.
Hind al Utaibah, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Imarati (UAE) naye pia ametuma ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter ambao mbali na kuuelezea uamuzi wa Bahrain na utawala wa Kizayuni wa kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia kuwa ni habari nzuri sana alidai pia kwamba hatua hiyo itasaidia sana kuleta ustawi na uthabiti katika eneo.
Wakati Misri na Imarati zimeunga mkono hatua ya Bahrain ya kufikia mapatano na utawala wa Kizayuni, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imelaani hatua hiyo na kusisitiza kuwa, uamuzi huo wa utawala wa Aal Khalifa wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel unaupa nguvu utekelezaji wa vipengele vya mpango wa kihaini wa Muamala wa Karne ambao lengo lake ni kuua ndoto na malengo matukufu ya Palestina.
Daud Shahab, mkuu wa masuala ya habari wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina, yeye mbali na kulaani hatua ya utawala wa Aal Khalifa ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni amebainisha kwamba, makubaliano hayo yanadhihirisha jinsi utawala wa Bahrain unavyoiabudu na kuitii Marekani.
Nchini Bahrain kwenyewe, harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo ya Al-Wifaq nayo pia imelaani hatua hiyo ya utawala wa Aal Khalifa na kusisitiza kuwa, wananchi wa Bahrain hawatayapuuza wala kuyasahau malengo matukufu ya Palestina.
Ikumbukwe kuwa utawala wa Bahrain umechukua hatua ya kusaliti malengo matukufu ya Palestina na Ulimwengu wa Kiislamu kwa kuamua kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, ukiwa umepita mwezi mmoja tu tangu Imarati pia kuchukua hatua kama hiyo ambayo imekosolewa vikali na kulaaniwa na makundi ya Palestina, nchi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi na shakhsia kadhaa wa kisiasa, kijamii na kidini kote duniani.../