Silaha za Marekani-Uingereza sababu ya kuendelea vita huko Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i63384-silaha_za_marekani_uingereza_sababu_ya_kuendelea_vita_huko_yemen
Kukaririwa madai yasiyo na uthibitisho na yasiyo na msingi dhidi ya Iran liimekuwa jambo la kawaida kwa tawala za kibeberu hususan Marekani katika miaka ya hivi karibuni.
(last modified 2026-08-23T03:05:00+00:00 )
Sep 12, 2020 21:52 UTC
  • Silaha za Marekani-Uingereza sababu ya kuendelea vita huko Yemen

Kukaririwa madai yasiyo na uthibitisho na yasiyo na msingi dhidi ya Iran liimekuwa jambo la kawaida kwa tawala za kibeberu hususan Marekani katika miaka ya hivi karibuni.

Hakuna shaka kuwa lengo la kuibuliwa propaganda kama hizi ni kuficha vyanzo vikuu vya vitisho na vita katika eneo la magharibi mwa Asia. Mfano wa karibuni kabisa katika uwanja huu ni kutajwa jina la Iran ndani ya ripoti ya Baraza la Haki za Binadamu kwenye orodha ya nchi zinazotuma silaha huko Yemen ambazo zimetajwa kuwa ndio sababu ya kuendelea maafa nchini humo. Madai hayo ni ya uwongo na hayana ushahidi wowote wa kuyathibitisha. 

Saudi Arabia na Imarati zikiwa chini ya muungano vamizi ulioundwa na nchi kadhaa za Kiarabu na kusaidiwa na Marekani, mwaka 2015 zilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya nchi maskini zaidi ya Kiarabu ya Yemen ili kumrejesha madarakani Abdu Rabbu Mansour Hadi, rais mtoro aliyekimbia nchi wa Yemen na kutaka kufanikisha malengo yao ya kisiasa.  

Rais mtoro wa Yemen, Abdu Rabbu Mansour Hadi  

Vita dhidi ya Yemen vimewasababishia mamilioni ya watu wa nchi hiyo mgogoro mkubwa wa njaa kiasi kwamba Umoja wa Mataifa umeitaja hali ya Yemen kuwa ni janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani. Aidha kuendelea vita dhidi ya wananchi madhlumu wa Yemen hakuna natija nyingine ghairi ya mauaji na fedheha kwa waanzilishi wa vita hivyo na hadi sasa tunashuhudiwa kufeli kwa muungano huo wa Saudia katika vita vya Yemen.

Iran kwa upande wake ililaani mashambulizi ya muungano vamizi wa Saudia tangu hapo mwanzo na imekuwa ikiunga mkono mchakato wa kisiasa huko Yemen na jitihada za Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa.  

Hata hivyo vinara wa vita vya Yemen wanaendelea kutolea madai yasiyo na msingi wowote dhidi ya Iran kwa lengo la kuuza silaha zaidi na wakati huo huo baadhi ya nchi za eneo la magharibi mwa Asia zimegeuka kuwa maghala ya silaha zinazonunuliwa kutoka Marekani na nchi nyingine zinazofaidika na mgogoro wa Yemen. Ripoti ya shirika la Oxfam inaeleza kuwa, kuanzia mwezi Januari mwaka 2015 hadi sasa serikali ya Kihafidhina ya Uingereza imetoa kibali cha kuiuzia Saudi Arabia silaha zenye thamani ya pauni bilioni 6.4 na imekuwa na nafasi kubwa katika kuwapatia mafunzo wanajeshi wa nchi hiyo.  

Andrew Smith mwakilishi wa ngazi ya juu wa Harakati inayopinga biashara ya silaha nchini Uingereza amesema: Hakuna shaka kuwa silaha za Uingereza na Marekani zimekuwa na nafasi haribifu huko Yemen. Tunachokishuhudia sasaq nchini Yemen ni biashara ya silaha licha ya nchi hiyo kusumbuliwa na janga la kibinadamu.   

 Uuzaji wa silaha za Marekani kwa Saudi Arabia mwaka 2016 hadi 2017 uliongezeka mara mbili kutoka dola bilioni 1.8 na kufikia dola bilioni 3.4. Ongezeko hilo kubwa limetokana na siasa za Trump hususan za kuikamua Saudi Arabia; ambapo akiwa katika ziara yake ya kwanza huko Riyadh, kiongozi huyo wa Marekani aliandaa mazingira ya kusainiwa makubaliano ya kuiuzia Saudia silaha zenye thamani ya dola bilioni 110. Hata hivyo waungaji mkono wa tawala hizo zinazouwa watoto sasa wanageuza kibao na kudai kuwa serikali hizo hazihusiki kivyovyote katika mauaji ya watoto huko Yemen wala katika maafa ya kibinadamu nchini humo. Hii ni katika hali ambayo silaha zinazotengenezwa katika nchi hizo zinatumika waziwazi katika kuwaua watu wa Yemen na kubomoa miundomsingi ya nchi hiyo. 

Maafa ya vita vya Saudia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen  

Kama alivyosema Saed Khatibzadeh Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran: Kutolewa madai kwamba Iran inatuma silaha nchini Yemen ni jambo la kushangaza hasa ikitiliwa maanani kiwango kikubwa cha silaha zinazotuumwa na  baadhi ya nchi za Magharibi huko Yemen ambazo wakati mwingine hufikia thamani ya mabilioni ya dola.

Saed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran 

Ikumbukwe pia mzingiro usio wa kibinadamu dhidi ya Yemen unazuia hata kufikishwa misaada ya kibinadamu ya Iran katika nchi hiyo.