NAM: Israel inapaswa kuondoka katika milima ya Golan
Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) imeutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uondoke katika ardhi za Syria za milima ya Golan unazozikalia kwa mabavu.
Shirika la habari la Sputnik limeripoti habari hiyo na kuinukuu jumuiya ya NAM ikisema katika sehemu moja ya tamko lake rasmi kwamba utawala wa Kizayuni unapaswa kuondoka kwenye milima ya Golan unayoikalia kwa mabavu kwani milima hiyo ni mali ya Syria.
Katika sehemu nyingine ya tamko hilo lililotolewa baada ya kikao cha NAM kilichofanyika kwa njia ya Intaneti, jumuiya hiyo ya nchi zisizofungamana na siasa za upande wowote imesema, wanachama wa NAM wanalaani hatua zote zinazochukuliwa na wanajeshi vamizi wa Israel za kuvuruga hali ya kisheria, kijiografia na kijamii ya milima ya Golan.
Kwa mujibu wa tamko hilo lililotolewa jana Jumamosi, utawala wa Kizayuni wa Israel unapaswa kuheshimu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na uondoke kwenye milima ya Golan ya Syria unayoikalia kwa mabavu.
Mwaka 1967, utawala wa Kizayuni wa Israel uliteka karibu kilomita 1200 za ardhi ya Syria katika milima ya Golan na baada ya kupita muda uliyaingiza maeneo hayo katika ardhi nyingine zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni zilizopachikwa jina la kupandikiza la eti Israel.
Jamii ya kimtaifa imekataa kabisa kutambua kuwa milima hiyo si mali ya Syria, na daima inasisitiza kuwa milima ya Golan itaendelea milele kuwa mali ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nalo limetoa maazimio kadhaa ya kuthibitisha kuwa utawala wa Kizayuni unaikalia kwa mabavu milima ya Golan ya Syria.