Yemen: Mateka wetu wamefikwa na mateso ya kila aina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64060-yemen_mateka_wetu_wamefikwa_na_mateso_ya_kila_aina
Mkuu wa timu ya mazungumzo ya serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen amesema, ameshtushwa na simulizi za kuhuzunisha na kutia uchungu zilizosimuliwa na mateka wa nchi hiyo walioachiwa huru kutoka kwenye kifungo cha muungano vamizi wa kijeshi wa Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 17, 2020 00:59 UTC
  • Yemen: Mateka wetu wamefikwa na mateso ya kila aina

Mkuu wa timu ya mazungumzo ya serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen amesema, ameshtushwa na simulizi za kuhuzunisha na kutia uchungu zilizosimuliwa na mateka wa nchi hiyo walioachiwa huru kutoka kwenye kifungo cha muungano vamizi wa kijeshi wa Saudi Arabia.

Muhammad Abdusalam alieleza masikitiko yake hayo jana Ijumaa katika mahojiano na televisheni ya Al Masirah baada ya kukamilika awamu ya pili ya ubadilishanaji wa mateka kati ya serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen na serikali ya nchi hiyo iliyojiuzulu ambapo alisema, muungano wa Saudia hautambui dini wala akhlaqi.

Abdusalam ameongeza kuwa, muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ndio unaobeba dhima ya mateka wanaougua maradhi, wenye lishe duni na waliofikwa na anuai za mateso.

Mkuu wa timu ya mazungumzo ya serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen ameashiria pia hafla ya kuwalaki mateka wa nchi hiyo na akabainisha kwamba, halfa hiyo imeongeza nguvu na ushujaa wa kambi ya ndani na kuthibitisha kuwa nyuma ya mateka hao kuna umma uliosimama pamoja nao ambao hautawaacha peke yao.

Baadhi ya mateka wakiamkiana na kukumbatiana na wapendwa wao

Muhammad Abdusalam vilevile ametangaza utayari wa serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen wa kuharakisha mchakato wa kushughulikia faili la mateka ili kuhitimisha mateso na machungu wanayopata wananchi wa Yyemen.

Siku ya Jumatano yalifanyika mabadilishano makubwa kabisa ya mateka kati ya serikali ya uokovu wa kitaifa ya Yemen na serikali ya nchi hiyo iliyojiuzulu ya Abdrabbuh Mansur Hadi inayoungwa mkono na Saudi Arabia, ambapo kundi la kwanza la mateka wa jeshi na wapiganaji wa kamati za kujitolea za wananchi liliwasili katika uwanja wa ndege wa Sana'a.

Awamu ya pili ya mabadilishano hayo ya mateka baina ya pande hizo mbili ilifanyika jana Ijumaa.../