Ayatullah Sistani: Ni haramu kuuza na kununua bidhaa za Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64072-ayatullah_sistani_ni_haramu_kuuza_na_kununua_bidhaa_za_israel
Ayatullah Sayyid Ali Sistani, Marja'a mkubwa wa Waislamu wa Kishia nchini Iraq ametoa fatwa akisisitiza kwamba ni haramu kuuza na kununua bidhaa za utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 17, 2020 07:03 UTC
  • Ayatullah Sistani: Ni haramu kuuza na kununua bidhaa za Israel

Ayatullah Sayyid Ali Sistani, Marja'a mkubwa wa Waislamu wa Kishia nchini Iraq ametoa fatwa akisisitiza kwamba ni haramu kuuza na kununua bidhaa za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tovuti ya ofisi ya Ayatullah Sistani imeweka mtandaoni, fatwa ya mwanachuoni huyo mkubwa akijibu swali kuhusu iwapo inaruhusiwa kuuza na kununua bidhaa kutoka kwa vituo ambavyo baadhi ya mapato yake yanatumika kuusaidia utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema, haifai kufanya biashara ya aina yoyote ya bidhaa za Israel pamoja na bidhaa za mashirika ambayo imethibitika kwamba yanauunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel.

Habari nyingine kutoka nchini Iraq inazinukuu duru za usalama za nchi hiyo zikitangaza habari ya kuangamizwa kiongozi wa genge la kigaidi na ukurufishaji la Daesh (ISIS), mkoani Kirkuk.

Brigedia Jenerali Yahya Rasool, Msemaji wa Komandi Kuu ya Majeshi ya Iraq

 

Televisheni ya al Alam imemnukuu Brigedia Jenerali Yahya Rasool, Msemaji wa Komandi Kuu ya Majeshi ya Iraq akisema leo (Jumamosi) kwamba kikosi cha kupambana na mgaidi cha nchi hiyo kimefanikiwa kumwangamiza mkuu wa magaidi wa Daesh katika operesheni iliyofana ya eneo la Wadi al Shai, kusini mwa mkoa wa Kirkuk.

Wakati huo huo kikosi cha taarifa za kijasusi cha jeshi la Iraq kimetangaza kuwa, kimezitia mbaroni familia za magaidi wa ISIS karibu na milima ya Sinjar, magharibi mwa mkoa wa Nainawa (Nineve). Familia hizo zilikuwa zimejipenyeza kwa siri nchini Iraq kutokea Syria.

Licha ya genge la kigaidi la Daesh kusambaratishwa nchini Iraq, lakini bado baadhi ya magaidi wa genge hilo wamejificha katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na hufanya vitendo vya kigaidi katika maeneo ya hapa na pale ya nchi hiyo.