Maher al Akhras, wafungwa wa Palestina na utawala wa Kizayuni
Zaidi ya siku mia moja zimepita tokea Maher al Akhras, mfungwa wa Kipalestina aanze mgomo wa chakula katika mojawapo ya jela za utawala haramu wa Israel na sasa maisha yake yamo hatarini kutokana na hali ngumu anayoipitia na vile vile udhaifu wa mwili wake.
Maher al Akhras aliye na umri wa miaka 49 amekuwa akizuiliwa jela tokea tarehe 27 Julai hadi sasa. Alianza kususia chakula kwa muda usiojulikana kwa ajili ya kulalamikia ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Kwa kutilia maanani kwamba mfungwa huyo wa Palestina amekuwa akisusia chakula kwa zaidi ya siku 100, amedhoofika sana kimwili na makundi tofauti ya Kipalestina yamekuwa yakiuonya utawala katili wa Israel dhidi ya kuruhusu mfungwa huyo afe shahidi. Utawala huo umekataa kumuachilia huru na inaonekana umeamua kufuata njia ya kuacha afe shahidi taratibu.
Siasa za kuwaua taratibu wafungwa wa Palestina zimekuwa zikitekelezwa kwa muda sasa na utawala huo ghasibu ambapo wafungwa wagonjwa wa Kiapalestina wameachwa kwa makusudi ili wafe taratibu. Tokea mwaka 1967 hadi leo yaani katika kipindi cha miaka 53 iliyopita, wafungwa 225 wa Kipalestina wamekufa shahidi wakiwa katika jela za kuogofya za utawala huo. Nuru al-Barghuthi mfungwa mwenye umri wa miaka 23, Sa'di al-Gharbi miaka 75 na Dawoud Tal'at al-Khatib mwenye umri wa miaka 45 ni wafungwa watatu wa Kiapalestina ambao wamepoteza maisha katika miezi 6 iliyopita kutokana na kunyimwa huduma za matibabu walipokuwa katika jela za utawala katili wa Israel. Utawala huo unatekeleza siasa za mauaji ya taratibu dhidi ya wafungwa wa Kipalestina kwa kutowapa matibabu ya dharura wanapokuwa katika jela zake.
Mai al-Kaila, Waziri wa Afya wa Palestina, ameonya kuhusu hali mbaya ya kimwili na kiafya ya Maher al-Akhras na kuongeza kuwa licha ya kuwa mfungwa huyo wa Palestina anakabiliwa na hali hatari na ya mara kwa mara ya mshtuko wa moyo, lakini utawala wa Kizayuni hauchukui hatua yoyote ya kumpa matibabu ya dharura.
Nukta muhimu kuhusu hali ya mfungwa huyo wa Palestina ni kuwa ana watoto 6 ambapo katika miaka ya 1989, 2004, 2009 na 2018 alikamatwa na kufungwa jela kwa jumla ya miezi 62. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa al-Akhras na familia yake ni nembo ya mapambano miongoni mwa Wapalestina. Ni kutokana na ukweli huo ndipo utawala wa Israel ukakataa kwa makusudi kumpa matibabu na kuamini kuwa kifo chake kitakuwa kwa maslahi ya utawala huo.
Jambo jingine ni kuwa kuna makumi ya Wapalestina ambao wanateseka na kuhatarishwa maisha yao katika jela za kuogofya za utawala huo wa kibaguzi. Wafungwa wa Kipalestina wapatao 80 wameambukizwa virusi vya corona katika jela hizo. Utawala huo unafurahia mwenendo wa kuwa na uhusiano wa kawaida na nchi kadhaa vibaraka za Kiarabu ambapo kimya cha nchi hizo na jamii ya kimataifa kinaupa fursa ya kuendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina.
Katika uwanja huo, Alam al-Ka'bi, mwanachama wa Kamati Kuu ya Mrengo wa Umma wa Palestina na ambaye anasimamia masuala ya wafungwa wa Palestina katika kamati hiyo amesema kwamba si mbali kuwa utawala huo inasambaza kwa makusudi virusi vya corona kati ya wafungwa wa Palestina ili uwatumie katika majaribio ya dawa zake za corona. Dhana hiyo inapata nguvu hasa kwa kutilia maani kwamba mashirika ya kutengeneza dawa ya utawala huo tayari yamethibitika kuwatumia wafungwa wa Kipalestina katika majaribio ya baadhi ya dawa zake.
Katika hali hiyo, ni wazi kuwa kufa shahidi Maher al-Akhras au mfungwa mwingine yeyote wa Kipalestina kutokana na uzembe wa kimatibabu wa utawala wa Kizayuni au kutokana na kukata tamaa Wapalestina kuhusu jamii ya kimataifa, kunaweza kuchochea machafuko na ghasia mpya kati ya Wapalestina na utawala wa Israel.
Kuhusu hilo viongozi wa mapambano ya Kiislamu ya Palestina wamesisitiza kuwa kuenea corona katika jela za Kizayuni na kuzorota afya ya Maher al-Akhras baada ya kupita zaidi ya siku 100 bila kula chakula, bila shaka kutaelekeza mapambano katika medani ya vita.