Saratani imekithiri Yemen kutokana na wavamizi kutumia silaha zilizopigwa marufuku
Waziri wa Afya wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema, idadi ya watu wanaougua maradhi thakili ya saratani nchini humo imeongezeka kutokana na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kutumia silaha zilizopigwa marufuku.
Taha al Mutawakil ameongeza kuwa, tangu Saudia na waitifaki wake walipoivamia kijeshi Yemen, idadi ya wagonjwa wa saratani katika maeneo yaliyoshambuliwa kwa silaha zilizopigwa marufuku imeongezeka kwa asilimia mia moja.
Al Mutawakil amebainisha kuwa, vituo vya tiba ya saratani ya damu nchini Yemen vinapokea wagonjwa elfu saba kwa mwaka kutoka mikoa mbalimbali ya nchi hiyo, ambapo nusu ya wagonjwa hao hufariki dunia kutokana na uhaba wa dawa na vifaa maalumu kwa ajili ya wagonjwa wa maradhi hayo.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ameeleza kwamba, Umoja wa Mataifa umeshindwa kuingiza nchini humo hata vifaa vya kawaida vya matibabu na ameukosoa pia utendaji dhaifu wa Shirika la Afya Duniani WHO nchini humo.
Moto wa vita uliowashwa na Saudi Arabia na watifaki wake tangu mwezi Machi 2015 nchini Yemen na kuendelea kuwaka hadi sasa umeshateketeza roho za watu zaidi ya elfu kumi na sita na kuwajeruhi makumi ya maelfu, mbali na mamilioni ya wengine walioalizimika kuwa wakimbizi.../