Saudia yairubuni Niger ianzishe uhusiano wa kawaida na Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64607-saudia_yairubuni_niger_ianzishe_uhusiano_wa_kawaida_na_wazayuni
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimetangaza kwamba sasa hivi kunafanyika mazungumzo ya siri baina ya utawala huo ghasibu na nchi ya Kiafrika ya Niger kwa ajili ya kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande mbili huku Saudi Arabia ikiwa mstari wa mbele kuwarubuni viongozi wa Niamey wakubali kuanzisha uhusiano huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 13, 2020 23:03 UTC
  • Saudia yairubuni Niger ianzishe uhusiano wa kawaida na Wazayuni

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimetangaza kwamba sasa hivi kunafanyika mazungumzo ya siri baina ya utawala huo ghasibu na nchi ya Kiafrika ya Niger kwa ajili ya kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande mbili huku Saudi Arabia ikiwa mstari wa mbele kuwarubuni viongozi wa Niamey wakubali kuanzisha uhusiano huo.

Televisheni ya al Alam imelinukuu gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth likitangaza habari hiyo na kusema kuwa, Niger ndiyo nchi kubwa zaidi ya Waislamu magharibi mwa Afrika. Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimetangaza katika wiki za hivi karibuni kwamba mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Mohamad bin Salman yuko mstari wa mbele katika kuwarubuni viongozi wa Niger wakubali kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu kama ambavyo Saudia imeunga mkono pia hatua za Imarati, Bahrain na Sudan za kutangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni.

Gazeti la Yedioth Ahronoth limegusia pia kuwa wizara ya mambo ya nje ya utawala wa Kizayuni ina matumaini makubwa kwamba Niger itakuwa nchi itakayofuatia ya Waislamu, kutangaza uhusiano wa kawaida na Israel.

Waarabu waliotangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni

 

Gazeti hilo limenukuu waziri wa intelijensia na ujasusi wa utawala wa Kizayuni, Eli Cohen, akisema kuwa, mapatano baina ya Israel na nchi za Waislamu barani Afrika yataleta utulivu wa kieneo na kwamba uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni huko Niger utakuwa muhimu sana katika mchakato wa kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande mbili hizo.

Aidha mchambuzi mmoja Mzayuni ameandika katika gazeti hilo kwamba utawala wa Kizayuni umepanga kutumia fursa ya kuwepo Donald Trump katika ikulu ya White House, kuanzisha uhusiano pia baina ya Wazayuni na Morocco kupitia kutambua Marekani umiliki wa Morocco wa eneo la Sahara Magharibi.