Ulimwengu waitaka Israel isimamishe mara moja ujenzi wa vitongoji vipya
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64682-ulimwengu_waitaka_israel_isimamishe_mara_moja_ujenzi_wa_vitongoji_vipya
Mpango wa utawala haramu wa Isreal wa kujenga nyumba mpya zaidi ya 1,200 katika ardhi za Wapalestina unazozikalia kwa mabavu, umeamsha tena hasira ya jamii ya kimataifa ambapo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab League, imeutaja mpango huo kuwa hatari kubwa inayopasa kushughulikiwa haraka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 17, 2020 09:05 UTC
  • Ulimwengu waitaka Israel isimamishe mara moja ujenzi wa vitongoji vipya

Mpango wa utawala haramu wa Isreal wa kujenga nyumba mpya zaidi ya 1,200 katika ardhi za Wapalestina unazozikalia kwa mabavu, umeamsha tena hasira ya jamii ya kimataifa ambapo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab League, imeutaja mpango huo kuwa hatari kubwa inayopasa kushughulikiwa haraka.

Akizungumzia suala hilo hapo jana Jumatatu, Said Abu Ali, naibu katibu mkuu wa jumuiya hiyo anayeshughulikia masuala ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel ameiomba jamii ya kimataifa ipinge wazi mpango huo unaofuatiliwa na utawala ghasibu wa Israel.

Ameitaka jamii ya kimataifa iwashinikize watawala wa Tel Aviv ili waachane na mpango wao huo ambao unatekelezwa kinyume kabisa na maazimio pamoja na matakwa ya Umoja wa Mataifa.

vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

Wizara ya Ujenzi wa Nyumba ya utawala haramu wa Israel ilitangaza mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba tayari ilikuwa imeanza kupokea tenda za ujenzi wa nyumba za Wazayuni zipatazo 1257 katika eneo la mashariki mwa mji mtakatifu wa Quds.

Ujenzi huo bila shaka utakata njia ya mawasiliano na kuwazuia Wapalestina kuingia katika mji huo ambao wanatazamia kuufanya kuwa mji mkuu wa taifa lao la baadaye.