Kamati za Muqawama Palestina: Watawala wa Bahrain wamelisaliti taifa la Palestina
Msemaji wa Kamati za Muqawama za Palestina amelaani vikali safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na zilizopewa jina bandia la Israel.
Abu Mujahid ambaye ni mmoja wa makamanda wa muqawama Palestina ametangaza kuwa, hatua ya watawala wa Baharain ya kuanzisha uhusiano wa kawaiada na utawala haramu wa Israel na viongozi wao kufanya safari katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni usaliti na khiana kwa Wapalestina na kadhia ya Palestina.
Abdullatif bin Rashid Al-zayani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain hivi majuzi aliongoza ujumbe wa ngazi za juu wa serikali ya Manama kuzitembelea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari akiwa pamoja na Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani pamoja na mwenyeji wao Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel, Abdul-Latif Rashid al-Zayani Waziri wa Mambo ya Nje wa Bahrain alisema kuwa, nchi yake imekubali ombi la Israel la kufungua ubalozi mjini Manama.
Tarehe 15 Septemba mwaka huu, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain walitia saini makubaliano ya kutangaza uhusiano wa kawaida baina ya nchi zao na utawala ghasibu wa Israel.
Mwezi uliopita pia viongozi wa Marekani, Sudan na utawala haramu wa Israel wametangaza katika taarifa yao pamoja juu ya kufikiwa makubaliano baina ya Tel-Aviv na Khartoum ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina yao.