Rais wa Russia asisitizia haki ya Wapalestina ya kupigania ukombozi wao
Rais Vladimir Putin wa Russia amemtumia ujumbe wa maandishi Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kushikamana na Taifa la Palestina na kusisitiza kuwa ni haki ya taifa hilo kupigania ukombozi wake.
Shirika rasmi la habari la Palestina la WAFA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, katika barua yake hiyo, Rais Vladimir Putin amesema, Russia muda wote inaunga mkono juhudi za kupata Wapalestina haki zao zote ikiwemo kuundwa nchi huru ya Palestina.
Aidha Rais Putin ametangaza kuunga mkono juhudi za kutafuta njia za kisiasa, za kiadilifu na za kudumu za kutatua kadhia ya Palestina kwa mujibu wa sheria za kimataifa akisisitiza kuwa, Moscow inaunga mkono fikra ya kuanza tena mazungumzo ya moja kwa moja baina ya Palestina na Israel.
Vile vile amesema, Russia ina nia ya kweli ya kustawisha uhusiano wa kiurafiki na Mamlaka ya Ndani ya Palestina na ushirikiano wa pande mbili katika nyanja tofauti.

Kwa upande wake, Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, Siku ya Kimataifa ya Kushikamana na Palestina ni siku iliyotangazwa kiuadilifu kwa ajili ya kuyakumbusha mataifa ya dunia haki walizoporwa na wanazoendelea kuporwa wananchi wa Palestina.
Abdul Latif al Kanou' amesema hayo na kuongeza kuwa, siku hii inaitaka dunia kulibakisha hai suala la Palestina, dhulma linayofanyiwa taifa la Palestina na mateso wanayoyapata Wapaelstina kila siku kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Aidha amesema, walimwengu wanapaswa kuitumia vilivyo Siku ya Kimataifa ya Kushikamana na Taifa la Palestina kuonesha mshikamano wao kwa kweli taifa hilo linalodhulumiwa mno na kwa makumi ya miaka sasa.