Utata mwingi kuhusiana na kupatiwa ufumbuzi mzozo wa mataifa ya Kiarabu
(last modified Sat, 19 Dec 2020 03:00:30 GMT )
Dec 19, 2020 03:00 UTC
  • Utata mwingi kuhusiana na kupatiwa ufumbuzi mzozo wa mataifa ya Kiarabu

Katika kipindi cha mwezi mmoja wa hivi karibuni kumekuwa kukiripotiwa habari kuhusiana na kupatiwa ufumbuzi mgogoro baina ya Qatar na mataifa manne ya Kiarabu ya Saudi Arabia, Imarati, Misri na Bahrain.

Hata hivyo hakuna mwafaka wa pamoja baina ya mataifa hayo manne.

Ikumbukwe kuwa tarehe 5 Juni mwaka 2017, Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri zilichukua hatua ya kuvunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar kwa sababu ya serikali ya Doha kutofuata muelekeo wa nchi za Kiarabu zinazoongozwa na Saudia. Lakini mbali na kuiwekea vikwazo Qatar, nchi hizo zilifungia pia Doha mipaka yao ya ardhini, baharini na angani.

Mnamo tarehe 23 Juni, 2017 nchi hizo nne ziliipatia Qatar orodha ya masharti 13 na kutangaza kuwa kurejeshwa tena uhusiano wa kawaida na nchi hiyo kutategemea utekelezwaji wa masharti yote hayo na serikali ya Doha.

Masharti muhimu zaidi ambayo Saudia na washirika wake waliishurutisha Qatar ni kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran na Hizbullah ya Lebanon, kuifunga stesheni ya televisheni ya Aljazeera na kuondoa kituo cha kijeshi cha Uturuki ndani ya ardhi ya Qatar.

 

Serikali ya Doha imeyakataa masharti hayo na kusema bayana kwamba, yanakiuka mamlaka ya kujitawala na kujiamulia mambo yake nchi hiyo. Katika kipindi cha miaka mitatu na nusu iliyopita, serikali ya Doha imefanikiwa kuvuka salama kipindi kigumu cha mashinikizo na kivitendo kuzisambaratisha njama na siasa za nchi hizo nne za Kiarabu dhidi yake.

Desemba kila mwaka kawaida hufanyika kikao cha wakuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Bado haijafahamika hasa kikao cha mwaka huu wa 2020 cha wakuu hao kitafanyika lini. Gazeti la Kuwait la al-Rai hivi karibuni lilinukuu vyanzo vya kidiplomasia vya ngazi za juu na kuandika, katika kikao kijacho cha wakuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kutafanyika upatanishi na maridhiano baina ya mataifa manne ya Saudi Arabia, Imarati, Misri na Bahrain na taifa la Qatar.

Kimsingi ni kuwa, ni Saudia na Qatar ndizo ambazo zimefikia baadhi ya makubaliano kwa ajili ya kutatua mzozo huo huku nchi nyingine zilizobakia zikiwa hazijaonyesha radiamali yoyote, jambo ambalo linaonyesha kuwa, hakuna kauli moja au mwafaka katika kadhia hiyo.

Viongozi wa Kiarabu ambao mataifa yao yameiwekea Qatar mzingiro

 

Radiamali ya kwanza ilionyeshwa na Imarati. Utawaa wa Abu Dhabu haujakaribisha makubaliano hayo, kwani yalifikiwa pasi na kuhudhuria wala kujulishwa nchi hiyo. Katika fremu hiyo, Abdul-Khaliq Abdallah, mshauri wa Muhammad bin Zayed al-Nahyan ambaye ni mrithi wa kiti cha ufalme wa Abu Dhabi ameandika katika ukurasa wake wa twitter akitoa majibu kwa habari zilizoenea za kuboreka uhusiano baina ya Riyadh na Doha: “Treni ya mapatano ya Ghuba (ya Uajemi) haitasogea hata sentimita moja endapo kutafikiwa makubaliano bila taarifa au mwafaka wa kabla.”

Baada ya Imarati, filihali Bahrain nayo imejitokeza na kutoa radiamali yake kuhusiana na mapatano ya Qatar na Saudia. Jumatano iliyopita ya Desemba 16, Bunge la Bahrain lilitoa taarifa likitaka kutofanyika mapatano na maridhiano ya Qatar na mataifa manne ya Kirabu yaliyoiwekea mzingiro nchi hiyo.

Sababu ya kutokuweko kauli na msimamo mmoja baina ya nchi hizo nne kuhusiana na kupatiwa ufumbuzi mgogoro baina yao na Qatar ni nini hasa?

Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani

 

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, sababu ya kwanza ni hatua ya Saudia ya kuyapuuza mataifa mengine katika mchakato wa makualiano na Qatar. Imarati imeashiria na kuzungumzia wazi wazi suala hilo, huku Misri ikiwa na wasiwasi wa kundi la Ikhwan kwani inaitambua Qatar kama muungaji mkono wa Ikhwanul Muslmiin na kwamba, uungaji mkono huo wa Doha kwa kundi hilo haujapungua.

Weledi wa mambo wanasema kuwa, sababu nyingine ni kwamba, kungali kuna hitilafu na Qatar katika nyanja nyingine. Bahrain ina hitilafu na Qatar kuhusiana na uvuvi wa samaki na haki za wavuvi na sababu ya taarifa ya Bunge la Bahrain Jumatano iliyopita inarejea katika kadhia hii. Rashid bin Abdallah al-Khalifa, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Bahrain ameituhumu Qatar kwamba, inachochea faili la mipaka yake kwa ajili ya kujitanua huku Bunge la nchi hiyo likisisitiza kuwa, serikali ya Manama haitafanya mapatano na suhulu yoyote ile na Doha kabla ya kupatiwa ufumbuzi matatizo na mivutano iliyopo baina ya pande mbili.

Tags