Malengo ya safari ya ghafla ya Saad Hariri nchini Uturuki
Saad Hariri, waziri mkuu mteule wa Lebanon ambaye amepewa jukumu la kuunda serikali, siku ya Ijumaa alifanya safari ya ghafla na ambayo haikuwa imetangazwa kabla kuelekea nchini Uturuki ambako alikutana na kufanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdoğan.
Moja ya sababu zilizoifanya safari ya Hariri nchini Uturuki iwe na umuhimu, ni kwamba nchi mbili za Saudi Arabia na Imarati, ambao ni waungaji mkono wake muhimu katika eneo zina mgongano wa kimaslahi na Uturuki na haziko tayari kuona Ankara inakuwa na ushawishi na satua katika Ulimwengu wa Waarabu. Katika mvutano wa ndani uliozuka baina ya Waarabu, kati ya Qatar na nchi nne za Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri, moja ya masharti ziliyotoa nchi hizo kwa ajili ya kurejesha uhusiano wao na Qatar ilikuwa ni nchi hiyo kuvunja au kupunguza kiwango cha uhusiano wake na Uturuki, sharti ambalo serikali ya Doha haikulikubali. Kwa upande mwingine, katika miezi ya karibuni, nchi za Kiarabu, na hasa Imarati imekuwa na uhusiano wenye mikwaruzano mikubwa na Uturuki. Jambo hili pia limezidisha umuhimu wa safari ya Saad Hariri mjini Ankara.
Nukta hiyo ina umuhimu katika upande mwingine pia. Wiki moja kabla ya safari ya Uturuki, Saad Hariri alifanya safari kuelekea Imarati; na huku akiwa na lengo la kuendelea na safari yake katika eneo kwa kuitembelea Saudia, safari hiyo ya Riyadh ilighairika. Hayakutolewa maelezo ya wazi kuhusu mazungumzo aliyofanya Hariri na viongozi wa Imarati, wala sababu ya kughairika safari yake ya Saudi Arabia, lakini inavyoonekana, waziri huyo mteule wa Lebanon aliyekabidhiwa jukumu la kuunda serikali mpya ya nchi hiyo hajapata uungaji mkono anaohitaji kwa serikali za Abu Dhabi na Riyadh. Na sababu kuu ni kwamba, Imarati na Saudi Arabia zimeonyesha zitakuwa tayari kumuunga mkono Hariri ikiwa atafanikiwa kuunda baraza la mawaziri litakalokuwa na wawakilishi wachache wa Hizbullah, wakati kiongozi huyo wa mrengo wa Al Mustaqbal anaelewa fika kuwa ni baidi kwake kuweza kufanikisha takwa hilo kwa kuzingatia hali ya sasa ya Lebanon na kwa kutilia maanani sauti kubwa na nafasi muhimu iliyonayo Hizbullah. Na ndio maana hata baadhi ya duru zimetangaza kuwa, Imarati na Saudi Arabia zinapanga kumfanya Baha Hariri, ndugu wa Saad Hariri, chaguo mbadala la kuunda serikali mpya ya Lebanon.
Nukta nyingine ni kwamba, safari ya Saad Hariri nchini Uturuki ina uhusiano wa moja kwa moja na uundaji serikali pamoja na matatizo ya kiuchumi ya Lebanon. Baada ya kupita miezi minne tangu Hariri alipoteuliwa kuwa waziri mkuu na kukabidhiwa jukumu la kuunda serikali, hadi sasa hajafanikiwa kukamilisha jukumu hilo. Hata Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah alisema katika hotuba aliyotoa siku ya Ijumaa iliyopita kwamba, mchakato wa uundaji serikali umekuwa tata. Inavyoonyesha, kwa safari aliyofanya nchini Uturuki na mazungumzo yake na rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdoğan, Hariri anajaribu kutafuta uungaji mkono kimataifa kwa ajili ya kuunda serikali mpya ya Lebanon. Kwa kuzingatia kwamba Uturuki haina ushawishi wa kisiasa ndani ya Lebanon, haitarajiwi kama itakuwa na msaada wa kutoa kufanikisha uundaji wa baraza jipya la mawaziri la nchi hiyo.
Pamoja na yote hayo, Uturuki ina uwezo mkubwa kiuchumi; na Lebanon inaweza kufaidika na uwezo na fursa za kiuchumi za nchi hiyo kwa ajili ya kuijenga upya Beirut. Mripuko uliotokea Agosti 4 mwaka jana katika mji mkuu huo wa Lebanon ulisababisha hasara ya karibu dola bilioni 15. Kwa kuzingatia matatizo mengi ya kiuchumi yanayoikabili Lebanon, kuna uwezekano mdogo wa kuweza kuukarabati mji mkuu wa Beirut kwa kutegemea vyanzo vya ndani vya fedha; hivyo nchi hiyo inalazimika kuomba misaada kutoka nje. Kuhusiana na suala hilo, ofisi ya Saad Hariri imeashiria katika taarifa kuhusu safari ya waziri mkuu huyo mteule nchini Uturuki na kutangaza kuwa, matatizo ya kiuchumi na kuanzisha mchakato wa ukarabati wa Beirut ilikuwa ndio ajenda kuu ya mazungumzo ya Hariri na Erdoğan.../