B'Tselem: Israel ni utawala wa kibaguzi
Kituo cha Haki za Binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) cha B'Tselem kimesema Israel ni utawala wa kibaguzi na wala si wa kidemokrasia.
Kituo hicho kimesema hayo leo Jumanne, hii ikiwa ni mara kwanza kwa taasisi hiyo kutoa tamko hilo dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, tangu kuasisiwa kwake miaka 31 iliyopita.
Taasisi hiyo imeeleza bayana kuwa, "Israel si utawala wa kidemokrasia, bali ni wa ubaguzi wa rangi (apartheid), na ambao kwa utaratibu maalumu unawakandamiza Wapalestina kwa kutumia nguvu za kijeshi na sheria za kibaguzi."
Kituo cha B'Tselem kimeongeza katika taarifa yake hiyo kuwa, utawala wa ubaguzi wa rangi wa Israel haukuzaliwa siku moja au kwa tamko moja, bali umepatikana katika mchakato ambao unaendelea kuwa mkubwa, na uliokubalika na kupata baraka za taasisi za utawala huo.
Hivi karibuni, B'Tselem ilisema mamia ya Wapalestina wameuliwa shahidi katika mipaka ya Ukanda wa Gaza kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Kizayuni kinyume cha sheria na bila ya sababu yoyote, na kwamba ufyatuaji risasi huo unatekelezwa na wanajeshi wa Kizayuni kwa idhini ya Mahakama Kuu ya utawala wa Kizayuni.
Kituo cha B'Tselem ambacho kinajishughulisha na upashaji taarifa kuhusu haki za binadamu huko Israel aidha kimeashiria kuwa duru nyingi rasmi za utawala wa Kizayuni zimekiri kwamba zinafahamu kuhusu kuuliwa wafanya maandamano wengi wa Kipalestina katika mipaka ya Gaza bila yoyote.