Ansarullah: Mazungumzo ya Yemen yatafanikiwa iwapo Saudia itasitisha vita
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i6670-ansarullah_mazungumzo_ya_yemen_yatafanikiwa_iwapo_saudia_itasitisha_vita
Harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah imesema ili mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Yemen yafanikiwe, sharti utawala wa Saudi Arabia usitishe mashambulizi yake mara moja.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 08, 2016 13:32 UTC
  • Ansarullah: Mazungumzo ya Yemen yatafanikiwa iwapo Saudia itasitisha vita

Harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah imesema ili mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Yemen yafanikiwe, sharti utawala wa Saudi Arabia usitishe mashambulizi yake mara moja.

Aamer Shane’e, mwanachama mwandamizi wa harakati hiyo katika mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa nchini Kuwait amesema kuwa, mazungumzo hayo hayatakuwa na tija yoyote iwapo utawala wa Aal-Saud utaendeleza uvamizi na hujuma zake nchini Yemen.

Aidha amesema kuna haja ya kukatwa misaada kwa makundi ya mamluki na makundi ya kigaidi yenye mafungamano na mtandao wa al-Qaeda nchini humo ili mazungumzo hayo yazae matunda.

Kadhalika harakati ya wananchi wa Yemen ya Ansarullah imeelezea kusikitishwa kwake na namna jeshi la Saudia linavyoendeleza mashambulizi yake ya kikatili licha ya mazungumzo hayo ya amani kuendelea. Ansarullah imesema kwa sasa jeshi hilo la utawala wa kifalme wa Aal-Saud linaendeleza hujuma za anga katika maeneo mengi ya Yemen kama vile mkoa wa Taiz, kusini magharibi mwa nchi.

Mazungumzo ya amani ya Yemen yenye lengo la kuhitimisha vita nchini humo yalianza terehe 21 ya mwezi uliopita wa Aprili huko nchini Kuwait chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo yameshindwa kuwa na tija kutokana na ukwamishaji unaofanywa kila mara na Saudia.