HAMAS: Mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza unaelekea kuvunjika
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema wananchi wa Palestina wamekaribia sana kuuvunja mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza uliowekwa na utawala wa Kizayuni tokea mwaka 2007.
Kiongozi wa HAMAS katika Ukanda wa Gaza, Yahya Sinwar alisema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake na ujumbe wa Misri uliozitembelea ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.
Sinwar amenukuliwa na shirika la habari la Ma'an akisema kuwa, wananchi wa Palestina wamejitoa muhanga kwa ajili ya kadhia yao muhimu ya kujikomboa toka kwenye mzingiro na uvamizi wa utawala haramu wa Israel.
Amesisitiza kuwa, mazingira ya sasa ya kimataifa yameegemea zaidi kwa upande wa maslahi ya taifa la Palestina, na fursa hii inapaswa kutumiwa kwa njia bora zaidi.
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amebainisha kuwa, taifa la Palestina linastahiki kuishi na kujivunia haki zake za msingi.
Kadhalika ametadharisha kuwa, wananchi wa Palestina wapo tayari kujibu aina yoyote ya uvamizi na chokochoko za utawala pandikizi wa Israel.