Hamas: Uhusiano na Iran ni wa muda mrefu na unaendelea
(last modified Mon, 05 Jul 2021 02:39:37 GMT )
Jul 05, 2021 02:39 UTC
  • Hamas: Uhusiano na Iran ni wa muda mrefu na unaendelea

Mwanachama mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema uhusiano wa harakati hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni wa muda mrefu na kusisitiza kuwa harakati hiyo pia inataka kuboresha uhusiano na Saudi Arabia na nchi zingine zote isipokuwa utawala bandia wa Israel.

Khalil Al Hayeh, naibu wa Ismail Haniya, Mkuuu wa Idara ya Kisiasa ya Hamas aliyasema hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa, uhusiano wa Hamas na Iran umekuwa imara kwa muda mrefu.

Kuhusu mazungumzo yake akiwa Lebanon, Al Hayeh amesema Hamas imefanya mazungumzo na kiongozi wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrallah kuhusu njia za ushirikiano kwa ajili ya kuwahudumia Wapalestina katika harakati zao za ukombozi na pia kuhusu  matatizo ya wakimbizi Wapalestina nchini Lebanon.

Afisa huyo mwandamizi wa Hamas amesema harakati hiyo inataka kuwa na uhusiano na wote na inawatahadharisha wale ambao wanataka kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mkutano wa Ismail Haniyah (kushoto) na Sayyid Hassan Nasrallah

Kuhusu uhusiano wa Hamas na Saudi Arabia amesema harakati hiyo inajaribu kuwa na uhusiano mzuri na ufalme huo. Amesema kukosekana uthabiti katika uhusiano wa pande hizo mbili kunatokana na mwenendo usio sahihi wa Saudia.

Wiki iliyopita Haniya alifika Beirut kwa lengo la kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu Lebanon na viongozi wa harakati za muqawama wenye makao yao Lebanon akiwemo Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrallah.

Ujumbe huo wa Hamas awali ulitembelea Morocco na Mauritania kabla ya kuwasili Lebanon.

Baadhi ya vyombo vya habari vimedokeza kuwa, baada ya Lebanon Ismail Haniya pia  atatembelea Iran na Uturuki.

Tags