Jeshi la Iraq laua viongozi kadhaa wa ISIS kaskazini mwa nchi
Idara ya Intelejensia na Upelelezi ya Iraq imetangaza habari ya kuangamizwa wanachama kadhaa wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika mkoa wa Kirkuk, kaskazini mwa nchi.
Katika taarifa, idara hiyo imesema wanajeshi wa Iraq wamefanikiwa kuangamiza wanachama kadhaa wa Daesh, wakiwemo viongozi wa ngazi za juu wa genge hilo la kigaidi, katika operesheni ya usiku wa kuamkia leo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vikosi vya Iraq vimeshambulia ngome na maficho ya wanachama hao wa ISIS, ambapo kadhaa miongoni mwao wameuliwa huku wengine wengi wakijeruhiwa.
Mikoa ya Kirkuk, Nainawa, Al Anbar, Diyala na Salahuddin huko kaskazini na magharibi mwa Iraq ni vituo vikuu vya mabaki ya magaidi wa kundi la Daesh (ISIS).
Jeshi la Iraq kwa muda sasa limekuwa likiendesha operesheni dhidi ya masalia na mamluki wa kundi la kigaidi la Daesh hususan katika maeneo ya mikoa ya Kirkuk, Salahuddin na Diyala maarufu kwa jina la " Pembe Tatu za Mauti."
Genge hilo la ukufurishaji kwa uungaji mkono wa hali na mali wa Marekani na waitifaki wake wa Magharibi na baadhi ya tawala vibaraka za Kiarabu liliivamia Iraq na kukaliwa kwa mabavu sehemu kubwa ya maeneo ya kaskazini na magharibi mwa nchi.
Hata hivyo mwaka 2017, jeshi la Iraq kwa msaada wa ushauri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilifanikiwa kukomboa mji wa Rawa katika mkoa wa al-Anbar magharibi mwa nchi hiyo ya Kiarabu, iliyokuwa ngome ya mwisho ya kundi la ISIS.