Taliban yakataa kushirikiana na Marekani katika mapambano dhidi ya Daesh
Kundi la Taliban limetangaza kuwa lina uwezo wa kutosha wa kupambana na kundi la kigaidi la Daesh na kwa msingi huo halitashirikiana na Marekani katika uwanja huo.
Akifafanua suala hilo, Suhail Shahin, ambaye amependekezwa na kundi hilo kuliwakilisha katika Umoja wa Mataifa amesema Taliban itapambana na Daesh bila kuushirikisha upande wa tatu na kwamba haina nia ya kushirikiana na Washington katika uwanja huo.
Hii ni katika hali ambayo baada ya Taliban kuteka Kabul, mji mkuu wa Afghanistan, Daesh imetekeleza nchini humo operesheni kadhaa za kigaidi ikiwemo ya karibuni katika msikiti wa Mashia wa Kunduz ambapo waumini 300 waliuawa shahidi na kujeruhiwa katika operesheni hiyo.
Sisitizo la Shahin ambaye ni kati ya viongozi wa ngazi za juu wa Taliban kuhusu kutoshirikiana kundi hilo na Marekani katika mapambano dhidi ya Daesh nchini Afghanistan ni ishara ya wazi kwamba kundi hilo halina nia ya kushirikiana na White House katika kudhamini usalama wa nchi hiyo. Tangu Taliban idhibiti hali ya mambo mjini Kabul tarehe 15 Agosti iliyopita, Daesh imetekeleza operesheni kadhaa za kigaidi katika pembe tofauti za Afghanistan na hivyo kuufanya utawala wa Taliban ukabiliwe na changamoto kubwa za kiusalama.
Licha ya kuwa Dhabihullah Mujahid, mmoja wa wasemaji wa Taliban amedai kuwa Daesh sio tishio kubwa kwa kundi hilo na usalama wa Afghanistan lakini mashambulio ya kigaidi ya karibuni ya kundi hilo, na hasa la kuuawa na kujeruhiwa mamia ya waumini katika msikiti wa Mashia wa Kunduz, yanathibitisha wazi kuwa Daesh bado ni tishio kubwa kwa usalama wa Afghanistan na hasa kwa jamii ya Mashia. Ni wazi kwamba kundi hilo linalenga kuvuruga usalama wa Afghanistan kupitia uchochezi wa kimadhehebu na kikabila.
Daesh ambayo inadai kuasisi serikali ya Kiislamu ya Sham na Iraq imeeneza ugaidi wake katika eneo ambapo nchi za Afghanistan na Pakistan pia zimewekwa katika ramani ya operesheni za kigaidi ya kundi hilo la kitakfiri. Daesh pia imeeneza sheghuli zake katika eneo la kusini mashariki mwa Asia ambapo harakati zake za kigaidi zinaonekana wazi katika nchi za eneo hilo zikiwemo Indonesia, Malaysia na Ufilipino. Kundi hilo limetokea kuwa moja ya makundi hatari zaidi ya kigaidi katika eneo hilo.
Katika hali ya hivi sasa ambapo utawala wa Taliban umeahidi kuwadhaminia Waafghani wote usalama wao, kuendelea ugaidi wa Daesh ni changamoto muhimu ya kiusalama kwa kundi hilo katika juhudi zake za kujaribu kurudisha utulibu na usalama katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita vya ndani na uvamizi wa wageni. Ni wazi kuwa iwapo ugaidi wa Daesh utaruhusiwa kuendelea huko Afghanistan hatimaye utaathiri na kudhoofisha nafasi ya Taliban miongoni mwa watu wa nchi hiyo. Ni kwa kuzingatia hilo ndipo karibuni viongozi wa Taliban wakatangaza kuwa wataanzisha operesheni kali za kukabiliana na magaidi wa Daesh katika pembe zote za nchi hiyo.
Kabla Taliban ichukue uongozi wa Afghanistan, kundi hilo liliichukulia Daesh kuwa kundi zuri la kigaidi lililoendesha harakati zake kwa ajili ya kukabiliana na serikali ya zamani ya nchi hiyo iliyoongozwa na Muhammad Ashraf Ghani, lakini baada ya kuangishwa serikali hiyo na Taliban kuchukua uangozi wa nchi, kundi hilo halina tena mtazamo huo kuhusu Daesh na sasa linaona kuwa ni jukumu lake kusimama na kupambana na Daesh inayohatarisha utawala wake nchini.
Taliban imekataa kushirikiana na Marekani katika kupambana na Daesh katika hali ambayo inaomba na kuishawishi White House iitambue rasmi na kukubali utawala wake huko Afghanistan. Inaonekana kuwa kundi hilo limechanganyikiwa na kukabiliwa na mgangano wa wazi katika muamala wake na Marekani baada ya nchi hiyo ya Magharibi kukalia kimabavu na kijeshi ardhi ya Afghanistan kwa muda wa miaka 20. Ushirikiano wa Taliban na Marekani unachukuliwa kuwa changamoto kuu ya utambulisho wa kundi hilo na wakati huo huo kutoshirikiana na Wamarekani pia kutaathiri vibaya kimataifa fursa ya kitambuliwa kwake rasmi na hivyo kuwa na matokeo mabaya kwa utawala wake nchini Afghanistan.