Sherehe za Umoja wa Yemen zagubikwa na hujuma za Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i7639-sherehe_za_umoja_wa_yemen_zagubikwa_na_hujuma_za_saudia
Sherehe za mwaka wa 26 wa kuungana Yemen mbili zimefanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Sana'a huku ndege za kivita zikipita juu ya eneo la sherehe hizo siku ya Jumapili.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 23, 2016 07:29 UTC
  • Sherehe za Umoja wa Yemen zagubikwa na hujuma za Saudia

Sherehe za mwaka wa 26 wa kuungana Yemen mbili zimefanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Sana'a huku ndege za kivita zikipita juu ya eneo la sherehe hizo siku ya Jumapili.

Sherehe za kitaifa za kuadhamisha kuungana maeneo ya kusini na kaskazni mwa nchi hiyo zilifanyika katika medani ya Al-Sabeen mjini Sanaa. Washiriki wa Sherehe hizo za kitaifa walikuwa na bendera za Yemen iliyoungana. Ikumbukwe kuwa Yemen Kusini na Yemen Kaskazini ziliungana mwaka 1990 na kuwa nchi moja.

Mbali na Sana'a mji wa Al-Baidhah wa kusini mwa Yemen pia umeshuhudia maandamano makubwa kwa mnasaba huo wa siku ya kitaifa ye Yemen. Washiriki wa sherehe hizo wamelaani vikali kuendelea hujuma na ukatili wa Saudi Arabia na Marekani dhidi ya nchi yao.

Aidha washiriki wa maandamano hayo wamepongeza mapambano ya watu wa Yemen dhidi ya hujuma ya kijeshi inayoongozwa na Saudia dhidi ya nchi hiyo.

Saleh Samad, Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Harakati ya Wananchi ya Ansarullah akihutubu katika maandamano ya Sana'a amesema umoja wa Yemen ni jambo ambalo liko katika moyo wa kila Myemen na kwamba makundi ya kisiasa nchini humo yanapata uhalali wao kutokana na umoja wa nchi.

Samad ameongeza kuwa, watu wa Yemen wanadiriki kiwango cha matatizo na changamoto za kisiasa nchini humo na wanaamini kuwa njia za kutatua matatizo hayo si kuvuruga umoja uliopo bali ni kufuatilia marekebisho katika mkondo wa umoja.

Mkuu wa Baraza la Kisiasa la Ansarullah, harakati ya wananchi wa Yemen, amesema suala la dharura hivi sasa ni kuwa macho Wayem wote mbele ya njama dhidi ya taifa hilo. Ametoa wito kwa wananchi kutotumbukia katika mtego wa njama za adui.

Afisa huyo wa Ansarullah amesema muungano wa kijeshi wa Saudia na Marekani ndio wahusika wakuu wa ukatili na unyama unaofanywa dhidi ya taifa la Yemen hasa katika mikoa ya kusini mwa nchi hiyo.

Ameongeza kuwa mamluki wa Saudia na Marekani wameivamia Yemen kwa lengo la kutekeleza njama za mabeberu.

Kwa upande wake Mohammad Ali Al Houthi, Mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen akizungumza kwa munasaba wa maadhimisho ya miaka 26 ya kuungana Yemen amesema nchi hiyo inalengwa na maadui na kwamba njia pekee ya kukabiliana na hujuma hiyo ni Wayemen kuungana.

Al Houthi ameashiria njama za mabeberu huko Yemen na kusema wale wanaojaribu kuisambaratisha nchi hiyo kupitia nguvu za kijeshi wamesahau kuwa Wayemen ni wanamapambano shupavu.

Kiongozi huyo wa Yemen amesema ana yakini kuwa Wayemen wataendelea kusimama kidete kukabiliana na wavamizi wa kigeni na kuongeza kuwa, maadamu taifa la Yemen linadumisha umoja, basi maadui watashindwa katika njama zao.

Kwingineko, Ali Abdallah Saleh, Mkuu wa Chama cha Kongresi ya Kitaifa Yemen ametoa taarifa kwa munasaba wa maadhimisho ya siku ya umoja wa Yemen, na kusema serikali ya Saudia inawatakia mabaya watu wa nchi hiyo. Rais huyo wa zamani Yemen ameonya kuwa leo si tu kuwa umoja wa Yemen uko hatarini bali pia uhuru wa nchi hiyo unalengwa kusambaratishwa.

Ali Abdullah Saleh amesema rais aliyejiuzulu wa Yemen, Abdu Rabuh Mansour Hadi anatumiwa na ukoo wa Aal Saud kuigawa vipandevipande Yemen. Amesema Saudi Arabia haitaki kuona watu wa Yemen wakishi kwa uhuru, kujitegemea na kwa heshima. Amebaini kuwa Saudia inatumia uwezo wake wote wa kijeshi na kifedha kuidhoofisha Yemen.

Ikumbukwe kuwa Saudia Arabia, kwa idhini ya Marekani, ilianzisha vita dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdu Rabuh Mansour Hadi.

Baada ya kupita zaidi ya mwaka mmoja tokea Saudia ianzishe hujuma hiyo ya kinyama dhidi ya Yemen, zaidi ya raia 9,000 wameuawa wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto huku miundo mbinu ya nchi hiyo ikiharibiwa. Katika upande mwingine, Saudia imeshindwa kufikia malengo yake na sasa imetumbukia katika matatizo makubwa ya kisiasa na kiuchumi kutokana na vita dhidi ya taifa la Yemen.