Marekani yaafiki kuiuzia Saudi Arabia makombora yatakayogharimu dola milioni 650
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i76556-marekani_yaafiki_kuiuzia_saudi_arabia_makombora_yatakayogharimu_dola_milioni_650
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema nchi hiyo imeafiki ombi la Saudi Arabia la kuuziwa makombora ya anga kwa anga pamoja na zana zinazohusika kwa thamani ya dola milioni 650.
(last modified 2026-05-05T14:43:53+00:00 )
Nov 05, 2021 04:17 UTC
  • Marekani yaafiki kuiuzia Saudi Arabia makombora yatakayogharimu dola milioni 650

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema nchi hiyo imeafiki ombi la Saudi Arabia la kuuziwa makombora ya anga kwa anga pamoja na zana zinazohusika kwa thamani ya dola milioni 650.

Wakala wa Ushirikiano wa Usalama wa Ulinzi wa Marekani umelitaarifu bunge la nchi hiyo la Kongresi kwamba uuzaji wa zana hizo za kijeshi "utaimarisha sera za nje na usalama wa taifa wa Marekani."

Hati ya uidhinishaji mauzo hayo ya silaha imeitaja Saudi Arabia kuwa ni "nchi rafiki" inayohesabika pia kuwa "nguvu muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kisiasa katika Asia Magharibi."

Kuidhinishwa mauzo ya makombora hayo ni ushahidi mwingine unaotilia shaka ukweli na mwamana wa serikali ya Joe Biden ambayo iliingia madarakani kwa ahadi ya kuja kukomesha na kuhitimisha vita vya Yemen.

Ikumbukwe kuwa, Machi 2015, Saudi Arabia, ikungwa mkono na Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu, ilianzisha uvamizi na mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen, sambamba na kuiwekea mzingiro wa ardhini, angani na baharini nchi hiyo masikini ya Kiarabu.

Moto wa vita uliowashwa na Saudia na waitifaki wake, hadi sasa umeshateketeza roho za makumi ya maelfu ya Wayemeni na kujeruhi makumi ya maelfu ya wengine, mbali na mamilioni waliolazimika kuwa wakimbizi.

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa maafa ya kibinadamu yanayoikumba Yemen ni makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa hivi sasa ulimwenguni.../