Shambaulio la kutiliwa shaka dhidi ya makazi ya Mustafa al-Kadhimi
Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq alinusurika kifo jana alfajiri kufuatia shambulio la kombora lililofanyika dhidi ya makazi yake mjini Baghdad.
Katika siku nne zilizopita, Iraq imeshuhudia mivutano mikubwa ya kisiasa. Ijumaa Wairaki walifanya maandamano ya kulalamikia namna uchaguzi wa bunge ulivyofanyika, ambapo kulizuka mapaigano baina yao na askari usalama yaliyopelekea waandamanaji kadhaa kuuawa na wengine kujeruhiwa. Baada ya tukio hilo baadhi walimtuhumu Waziri Mkuu al-Kadhimi kuwa alihusika kwa njia moja au nyingine katika mapigano hayo na kuwa alituma vikosi maalumu vya askari kwa ajili ya kukandamiza waandamanaji. Masaa 48 baada ya tukio hilo habari ya kushambuliwa nyumba yake kwa ngege isiyo na rubani iliripotiwa ambapo waziri mkuu mwenye alithibitisha ukweli wa habari hiyo.
Shambulio hilo la droni ni la kutiliwa shaka kutokana na sababu kadhaa.
Ya kwanza ni kuwa lilipelekea kufunikwa na kusukumwa pembeni mapigano ya Ijumaa ambapo watu kadhaa waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Shambulio hilo lilipelekea kufunikwa sauti ya waandamanaji na badala yake kuangaziwa pakubwa shambulio hilo la kombora. Kwa msingi huo ni wazi kuwa waliohusika na mashambulio dhidi ya waandamanaji watasahaulika na kutofuatiliwa kisheria.
Sababu ya pili ni kwamba kufuatia shambulio hilo, makundi ya mapambano ya Iraq ndiyo yameelekezewa lawama na tuhuma za shambulio hilo, makundi ambayo yamekuwa katika mstari wa mbele wa kulalamikia matokeo ya uchaguzi wa bunge wa karibuni. Kufuatia mapigano ya Ijumaa baina ya waaandamanaji na askari usalama, baadhi ya viongozi wa Iraq akiwemo Qais al-Khazali, Katibu Mkuu wa mrengo wa Aswaib Ahl al-Haq wa Iraq walitangaza kuwa mapigano hayo yaliibuliwa ili kuyatuhumu makundi ya mapambano. Kwa msingi huo ni wazi kuwa kuna uhusiano na mfungamano wa moja kwa moja kuhusu matukio yanayoendelea hivi sasa katika nchi hiyo.
Dalili ya tatu katika uwanja huo ni kwamba shambulio dhidi ya nyumba ya al-Kadhimi linaweza kutumiwa vibaya kuzidisha ukandamizaji dhidi ya waandamanaji wanaolalamikia matokeo ya uchaguzi wa bunge kwa kuwa licha ya kwamba maandamano hayo ni ya amani lakini wapinzani wanaona kuwa yanachochea ghasia na kuhatarisha usalama wa Iraq. Kwa maneno mengine ni kuwa maandamano hayo yanaweza kutumiwa vibaya na maadui na hivyo kuhatarisha usalama na uthabiti wa Iraq, jambo ambalo linafuatiliwa kwa karibu na wapinzani wa makundi ya mapambano. Tunaona wazi mfano wa jambo hilo huko Lebanon. Wapinzano wa mrengo wa mapambano wanafanya kila wanaloweza kuvuruga usalama wa Lebanon ili isitawalike kidemokrasia na kwa mujibu wa matakwa ya wananchi. Kutokuwepo serikali imara na thabiti katika nchi za Lebanon, Iraq na Syria ni takwa muhimu la wapinzani wa mapambano.
Dalili ya nne ni kwamba mivutano inaendelea kuongezeka nchini Iraq huku kipindi cha kuondoka askari vamizi wa Marekani kikikaribia. Kwa mujibu wa mapatano ya al-Kadhimi na Rais Biden wa Marekani askari vamizi wa nchi hiyo wanapasa kuondoka Iraq ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Pamoja na hayo lakini Marekani inatumia mbinu tofauti ili iendelee kubakia kijeshi nchini humo. Hivyo kuvurugika usalama wa Iraq inaweza kuwa fursa nzuri kwa ajili ya kubakishwa nchini humno majeshi ya Marekani.
Kwa kutilia maanani dalili hizo, ni wazi kuwa lengo la kufanyika shambulio la kombora dhidi ya nyumba ya al-Kadhimi, ni la kutiliwa shaka. Katika uwanja huo huo, Abu Ali al-Askari, mkuu wa kitengo cha masuala ya usalama wa Kataib Hizbullah ya Iraq aliandika karibuni katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Telegram kwamba tukio la kushambuliwa kwa kombora nyumba ya al-Kadhimi mjini Baghdad ni la kimaonyesho tu kwa hoja kuwa hakuna yeyeto nchini Iraq aliye na hamu ya kupata hasara hata kama ni ya droni moja tu kwa kulenga nyumba ya Waziri Mkuu.