Hatua mpya ya Biden ya kuibua mvutano Ulaya Mashariki
Rais Joe Biden wa Marekani Jumatano alikubali kupeleka wanajeshi 3,000 huko Ulaya Mashariki na Ujerumani. Wanajeshi 1,700 wa Marekani wanatarajiwa kutumwa Poland na wanajeshi wengine 1,000 wa Marekani walioko Ujerumani kutumwa Romania. Wanajeshi 3000 zaidi watatumwa kutoka Marekani kwenda Ujerumani.
Pia kwa mujibu wa maelekezo ya Biden, Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, inapanga kuongeza idadi ya wanajeshi wa Marekani walioko Ulaya Mashariki hadi zaidi ya askari 8,500. Msemaji wa Pentagon John Kirby alisema Jumatano kwamba ahadi ya Marekani kwa NATO chini ya kifungu cha 5 cha Mkataba wa NATO ingalipo, na kwamba kama sehemu ya ahadi hiyo, hivi karibuni Merikani itahamishia wanajeshi zaidi nchini Romania, Poland na Ujerumani ili kujiandaa kwa lolote lile. Akieleza kuwa hali ya sasa inalazimu kuimarishwa nafasi ya NATO ya kuzuia hujuma ya adui mashariki mwa Ulaya, msemaji wa Pentagon amefafanua kuwa lengo la kutumwa askari katika maeneo yaliyotajwa ni kuongeza uwezo wa kiulinzi katika nchi washirika ambazo ziko mstari wa mbele.
Msemaji wa Ikulu ya White House Jen Saki alisema baada ya Pentagon kutangaza kuwa rais ameamua kutuma wanajeshi wa Marekani wapatao 3,000 Ulaya Mashariki, kwamba wanajeshi hao hawatakwenda Ukraine kwa ajili ya kupigana.
Agizo hilo jipya la Biden linalenga kutuma wanajeshi 3,000 Ulaya Mashariki kama sehemu ya msururu wa hatua za Marekani za kuleta mvutano Ulaya Mashariki na kuongeza makabiliano na Russia. Katika wiki za hivi karibuni, Washington kwa makusudi imeendesha vita vya kisaikolojia na kipropaganda dhidi ya Russia na ikishirikiana na NATO, daima imekuwa ikieneza propaganda chafu kuwa Russia inapanga kuivamia Ukraine. Lengo la Washington ni kuandaa mazingira ya kupelekwa askari zaidi wa Marekani na NATO Ulaya Mashariki na hivyo kupuuza matakwa ya kiusalama ya Russia. Ni wazi kuwa hatua hiyo inaongeza uwezekano wa kutokea mapigano kati ya Russia na NATO Ulaya Mashariki.
Moscow inataka kuhakikishiwa na Magharibi kwamba Ukraine haitajiunga na NATO, na kwamba vikosi na zana za kivita za NATO hazitatumwa karibu na mipaka ya Russia. Bila shaka, Marekani na NATO zimetoa majibu hasi kwa matakwa hayo yote mawili ya Moscow, jambo ambalo bila shaka limewakasirisha sana viongozi wa Russia.
Rais Vladimir Putin wa Russia alisema Jumanne: "Moscow haijapata jibu sahihi na la kuridhisha kutoka kwa Merikani na NATO kuhusu matakwa yake makuu matatu ambayo ni kutopanuliwa NATO upande wa Mashariki, kuepuka kupelekwa mifumo ya silaha za hujuma karibu na mpaka wa Russia na kurudishwa miundombinu ya kijeshi ya NATO barani Ulaya katika hali iliyokuwepo kufikia mwaka 1997."
Russia inaamini kuwa kutumwa mifumo ya Marekani ya kuzuia makombora nchini Romania na Poland kunatishia usalama wake.
Jambo jingine muhimu ni kwamba ingawa utawala wa Biden hapo awali ulisisitiza juu ya uwezekano wa Russia kuishambulia Ukraine wakati wowote lakini kwa sasa imepunguza propaganda hiyo chafu.
Jen Saki, Msemaji wa White House amesema: Washington kwa sasa haitasema kuwa kuna uwezekano wa kufanyika karibuni mashambulizi ya kijeshi ya Russia dhidi ya Ukraine, ingawa serikali ya Marekani bado inaamini kuwa mashambulizi hayo yanaweza kufanyika wakati wowote. Tumeacha kutumia ibara hiyo kwa sasa kwa sababu ilikuwa inafikisha ujumbe tofauti na ule tuliokuwa tumeukusudia mwanzoni.
Matamshi hayo yanaonyesha wazi kuwa, sio tu kwamba hakuna maafikiano kati ya maafisa waandamizi wa kijeshi na kisiasa wa Marekani kuhusu muda wa madai ya Russia kuivamia Ukraine, bali Washington imekiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba madai hayo hayana msingi wowote. Hii ni kwa sababu kupita muda mrefu na kutothibiti madai ya Marekani, kumeharibu itibari ya Washington na kuipelekea kutiliwa shaka katika ngazi za kimataifa.